Habari za Kitaifa

Hoteli kulipa familia ya mtalii aliyekufa katika mbuga ya Maasai Mara Sh23m

March 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SAM KIPLAGAT

HOTELI ya Keekorok Lodge imeagizwa na Mahakama Kuu ilipe familia ya mtalii Luo Jinli, raia wa China, Sh23 milioni kama fidia kufuatia kifo chake kilichotokea mwaka 2016.

Mtalii huyo alidungwa kisu na mtalii mwenzake waking’ang’ania nafasi kwenye meza wakati wa chakula cha alasiri baada ya kurejea hotelini baada ya matembezi katika mbuga ya wanyamapori ya Maasai Mara, Kaunti ya Narok.

Marehemu Luo na mumewe Dong Yi, walikabiliwa na Lee Changpin.

Lee aliwashambulia kwa kisu cha kukata nyama mle hotelini.

“Luo na Lee walitofautiana kuhusu mahala pa kukaa mle hotelini. Huku akijawa na hasira za mkizi, Lee aliwashambulia Luo na mumewe Dong kwa kuwadunga na kisu kifuani. Wote waliuguza majeraha mabaya kifuani,” jaji Francis Gikonyo alisema akitoa uamuzi.

Dong aliwashtaki wasimamizi wa hoteli hiyo iliyoko mbugani Maasai Mara, ambayo ni mojawapo ya hifadhi ya wanyamapori maarufu zaidi duniani kwa kutoweka tahadhari na kuajiri maafisa wa usalama kuhakikisha hali ni shwari mle ndani.

Luo aliaga dunia mnamo Agosti 8, 2016, baada ya kushambuliwa na Lee.

Dong aliuguza majeraha wakati wa kisa hicho.

Akitoa ushahidi kupitia kwa wakili Conrad Maloba, Dong alisema mshambuliaji wao hakuzuiliwa na maafisa wa usalama wa hoteli hiyo.

Ushahidi uliowasilishwa mbele ya jaji Gikonyo ulibaini kabisa kwamba wasimamizi wa hoteli hiyo walilegea kwa vile wangezima kisa hicho.

Kabla ya kifo chake, Luo, aliyekuwa na umri wa miaka 45, alikuwa ameajiriwa kama Meneja wa Usalama wa kampuni moja jijini Beijing.

Alikuwa ameandamana na mumewe Dong wakati wa ziara hiyo katika mbuga hiyo.

Walipowasili Maasai Mara, walikodisha chumba cha kulala kwenye Sun Africa Hotels inayofanya biashara ikitumia jina Keekorok Lodge Maasai Mara.

Luo na Dong pamoja na watalii wengine walikuwa wakitembezwa na mwelekezi wao Bw Bai Jiang.

Ziara yao iliharibika wakati wa kula chakula pale Lee alianza kumfokea Luo.

Lee alikuwa ameshika kisu cha kukatia nyama.

Ni kisu hicho ndicho alichokizamisha kifuani mwa Luo.

Dong alipoona mkewe amekabiliwa, alijaribu kuingilia kati kutuliza hali lakini bahati haikuwa upande wake, naye pia alishambuliwa na kujeruhiwa.

Katika uamuzi wake Jaji Gikonyo alisema hoteli hiyo iko na makosa kwa vile hakuajiri maafisa wa usalama kuhakikisha usalama wa watalii upo.

Alisema Dong aliyeshtaki hoteli hiyo amethibitisha kwamba usalama wake na wa mkewe aliyekuwa anapokea Sh2 milioni kwa mwaka haukuzingatiwa na hoteli.

Jaji Gikonyo alisema vurugu hotelini huchipuka na kwamba ni jukumu la wasimamizi wa hoteli kuhakikisha kuna maafisa wa kushika doria mle ndani.

Mbali na doria, maafisa hawa wa usalama huwahoji watalii kwa gumzo hapa na pale kujua kama “mambo ni bambam”.

Hoteli hiyo ilijitetea ikisema kwamba watalii hao kutoka China walizozana kwa lugha ya Kichina na ilikuwa jukumu lao kueleza usimamizi kwamba kulikuwa kumezuka hitilafu baina yao ili suluhu isakwe.

Baada ya kusema hayo. jaji huyo aliagiza hoteli imlipe Dong Sh100,000 kwa machungu aliyopata.

Pia iliagizwa imlipe Dong Sh21.5 milioni na Sh727,000 kama gharama maalum.