Habari za Kitaifa

Jowie atoa wimbo tarehe ya adhabu ikisogezwa

March 8th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA mara nyingine Joseph Irungu almaarufu ‘Jowie’ ametoa wimbo mwingine baada ya kikao cha mahakama.

Mara baada ya mahakama kuahirisha tarehe ya kutoa hukumu dhidi yake katika kesi ya mauaji ya Monica Kimani, Jowie alitoa kibao ‘I Believe’.

Kibao hicho ambacho tafsiri yake kwa Kiswahili ni ‘Naamini’, kinarejelea Zaburi 56:3, inayosema: “Nitakapokuwa na wasiwasi, nitakuamini. Haijalishi mitihani ya maisha utakayopitia, mwamini Mungu, kwani ndiye tegemeo pekee. Amini tu.”

Jowie alitoa wimbo huo dakika chache baada ya Jaji Grace Nzioka kuahirisha hukumu hadi Machi 13, 2024.

Jowie alipatikana na makosa ya kumuua Monicah, kufuatia uamuzi uliotolewa na mahakama mnamo Februari 9, 2024.

Mshtakiwa mwenzake, mwanahabari Jackie Maribe, aliondolewa mashtaka hayo baada ya kutopatikana na hatia yoyote.

Kwenye uamuzi wake, mahakama ilisema kuwa Jowie alipatikana na hatia ya mauaji hayo ambayo yalitekelezwa mnamo Septemba 19, 2018.

Sadfa ni kwamba, baada ya mahakama kumpata na hatia ya mauaji, Jowie alitoa wimbo unaoitwa ‘Nakuabudu’.

Wimbo huo unapoanza, Jowie anaimba kwamba atamsifu na kumheshimu Yesu.

Baadhi ya mistari iliyo kwenye wimbo huo ni “Nakuabudu, nakusujudu, ni wewe… Yesu Milele.”

Jowie pia aliambatanisha wimbo huo na nukuu kutoka kwa Biblia: Zaburi 150: 6 inayosema: “Acha kila kitu chenye uhai Kimsifu Bwana. Msifuni Bwana”.

Jowie alijitosa kwenye tasnia ya muziki mnamo 2020, kupitia wimbo wake wa kwanza ‘Nishikilie’.

Alitoa wimbo huo baada ya kuzuiliwa kwa muda katika Gereza Kuu la Kamiti. Alitoa wimbo huo baada ya kupewa dhamana na mahakama.

Ana nyimbo nyingine tatu ambazo ni: Babie’, ‘Eyaa’ na ‘Juu’ ambapo zote ni za injili.

Alikuwa mwanachama wa bendi iliyowaburudisha watu katika miji ya Naivasha na Nakuru, alikozaliwa na kulelewa.

Kulingana na baadhi ya marafiki wake wa utotoni, alianzisha safari yake ya uamuziki katika Kanisa la Agape, lililo katika mtaa wa Pangani, mjini Nakuru.