Makala

Walinzi wawili waumizwa na wezi wa mananasi ya Del Monte

March 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

WALINZI wawili wa kampuni ya G4S waliokuwa wakishika doria katika shamba la mananasi la kampuni ya Del Monte, wamelazwa hospitalini baada ya kuvamiwa na genge mnamo Ijumaa.

Genge hilo lilijumuisha vijana zaidi ya 70 kulingana na makadirio ya walioshuhudia.

Wahalifu hao walikuwa wamejihami kwa vifaa butu.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na kamati ya usalama ya Kaunti ndogo ya Ithanga/Kakuzi ikiongozwa na Kamanda wa polisi Bw Thomas Mong’are, nia ya genge hilo ilikuwa ya kuiba mananasi.

Wizi ambao hutekelezewa kampuni hiyo ya Del Monte ambayo hukuza mananasi katika shamba la ukubwa wa ekari 28,000 umekadiriwa kuwa wa kati ya Sh7 milioni na Sh10 milioni kwa mwezi mmoja.

“Walinzi hao wa G4S waliokuwa 20 na wakiwa wameweka ulinzi katika kipande cha ardhi iliyo chini ya upanzi wa mananasi kikifahamika kama ‘Field 47’ walivamiwa mwendo wa saa 12 jioni na genge hili,” ripoti hiyo yasema.

Inaongeza kwamba vijana hao walifanikiwa kutwaa gari moja la doria kutoka udhibiti wa dereva wa kampuni hiyo ya G4S na katika harakati za kujaribu kuhepa nalo, likagongana na pikipiki iliyokuwa ikiendeshwa na mwanachama mmojawapo wa genge hilo.

Soma Pia: Del Monte yasajili G4S kulinda mananasi kwa mazingira ya kuheshimu haki za binadamu

Ilibidi walinzi hao wa G4S kukimbilia maisha yao, nalo gari lao likiishia kuanguka na kubingiria.

Genge hilo lilibakia likiiba mananasi bila wa kuliuliza na likayatoa shambani humo na kuhepa nayo.

Wiki iliyopita, kampuni hiyo ya Del Monte iliwafuta walinzi wake 270 na kuingia katika mkataba na kampuni hiyo ya G4S ya kutuma walinzi 270 ili kusaidia kuweka ulinzi.

Katika taarifa iliyotolewa na kampuni ya Del Monte, walinzi wa G4S walisajiliwa ili kuleta nidhamu katika harakati za usalama baada ya hao wa awali kuaibisha kampuni hiyo mara kwa mara kupitia visa vya mauaji dhidi ya vijana ndani ya magenge hayo ya wizi wa mananasi.

Mauaji hayo yaliishia kuangaziwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, baadhi ya masoko ulimwenguni nayo yakitangaza marufuku ya uteja wao kwa bidhaa za Del Monte.

Vilevile, mtafaruku huo umeishia hata wakuu wa kiusalama wa Kenya kushtakiwa katika mahakama kuu ya Thika kwa madai kwamba wamelemewa kushinikiza kampuni ya Del Monte kuheshimu haki za binadamu.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Murang’a Kainga Mathiu ametangaza ushirika na kampuni hiyo ya Del Monte chini ya wito ‘Operesheni Linda Mananasi’ ambapo maafisa wa usalama watasaidia katika kuzima harakati za magenge hayo kuiba mananasi na kuzua hali za makabiliano ya mauti.

Bw Mathiu alisema kwamba harakati hizo zitapigwa jeki na huduma za ujasusi ili kuzima uhalifu unaotekelezwa.