Habari za Kitaifa

Tanzia: Kachero John Kamau kukumbukwa kwa kumkamata daktari feki

March 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

KACHERO John Njoroge Kamau aliyeaga dunia Ijumaa atakumbukwa kwa kuongoza kikosi cha polisi kilichovamia kliniki ya daktari bandia Mugo wa Wairimu katika mtaa wa Githurai 44 mwaka wa 2018.

Bw Kamau ambaye familia yake ilisema alifariki akiwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi baada ya kuugua homa ya mapafu, aliendesha operesheni kali alipokuwa hai.

Alikuwa na mchango muhimu polisi aliokuwa akiwaongoza walipomkamata Mugo ambaye baadaye alipatikana na hatia ya kuwapooza wanawake waliofika kwake kutibiwa na kuishia kuwabaka wakiwa hoi.

Mnamo Novemba 21, 2022, Mugo alihukumiwa kifungo cha miaka 29 gerezani baada ya kupatikana na hatia.

Maafisa waliofanya kazi na mwendazake katika uhai wake walimtaja kama mchangamfu na pandikizi la mtu ambaye kwa ujasiri mkuu alikuwa anatumia nguvu alizokuwa amejaliwa kuwafunga pingu wahalifu wasumbufu.

Ripoti za mashirika ya kutetea haki za binadamu hudai alikuwa anatumia nguvu kupita kiasi.

Familia ya kachero Kamau ilimuomboleza mwendazake ambaye ni mzawa wa Murang’a ikimtaja kama mwadilifu, mkarimu, mpenda watu na mwenye utu.

Ilisema alikuwa kiungo thabiti cha ustawi wa kijamii mashinani.

Mnamo mwaka 2017 Kamau anakumbukwa kama afisa aliyepambana sana na vurugu za mrengo wa upinzani–CORD– jijini Nairobi baada ya uchaguzi mkuu mwaka huo.

 

Kachero John Njoroge Kamau (kushoto) akisalimiana na aliyekuwa naibu kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Kimani Ruo mwaka wa 2007 ambaye muda mfupi baadaye alitoweka na hajawahi kupatikana. PICHA | MAKTABA

Lakini mwendazake pia mnamo mwaka 2007, alihusishwa na kutoweka kwa aliyekuwa naibu kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Kimani Ruo ambaye hadi leo hajawahi kupatikana. Ukweli wa kilichotokea haujafahamika hadi sasa.

[email protected]