‘Hakuna ruhusa sehemu ya ibada ukitoka kwa ngono’
NA FRIDAH OKACHI
ITAKUWAJE, umefika sehemu ya kufanyia ibada lakini wasimamizi wanakurudisha nyumbani kwa sababu umeonana kimwili na mchumba au mpenzi wako?
Msimamizi wa sehemu ya ibada Ngando, Dagoretti–yenye mti wa mugumo–Bi Nyambura Wahu, anasema ukiwa umeonana kimwili na mpenzi au mchumba wako siku hiyo, huna ruhusa kufika eneo hilo takatifu kwa mujibu wa imani yao.
Katika boma hilo lenye mti huo uliopewa hadhi kubwa, hakuna kuingia hapo ukitoka kwa ngono.
Pale, kuna malango mawili. Lango kubwa la sehemu ya ibada ni maalum na pale kuna masharti makali.
Anasema pale kwa mugumu panastahili kuwa safi na wanaotumia sehemu hiyom hawafai kivyovyote wawe wameonana kimwili. Isitoshe, mwanamke katika siku zake za mwezi naye anazuiwa.
Kulingana na Bi Wahu, hapo kwa mti Mungu huwasikiliza sana watu wa jamii ya Agikuyu.
Hapo kupiga kupiga kelele au kuingia na vyombo vya muziki kama vile ngoma hakufai.
“Mungu hataki kelele bali anataka kusikia kile wewe mja unachomweleza. Ile ni sehemu ya kunyenyenyekea na kusikiliza jinsi anavyosema kwa kuwa huzungumza,” akaeleza.
Kwa anayetaka kumuona Bi Wahu, analazimika kutumia lango la pili. Upande huo ikiwa ni sehemu yake ya kuishi.
Lango la kwanza hufunguliwa kukiwa na sherehe spesheli ambapo anaweza kukuruhusu upitie lango hilo.
“Lango la kwanza siwezi kukuruhusu kupitia… labda wakati wa sherehe zetu za kila mwaka ambazo hufanyika mara moja. Hiyo ndio siku ambayo tunaruhusu watu wengine kuingia… hata ambao si wafuasi wetu,” akasema.
Anasema sababu kuu ya kukosa kuruhusu kila yeyote yule, ni sehemu iliyotakaswa na uchafu wowote hata kwa wafuasi wake, ni marufuku.
“Ukiwa katika hali ile ya kwamba umeonana kimwili na mchumba wako, utakuwa unaenda kumuona Mungu ukiwa na uchafu,” akasema huku pia akionya wanawake walio katika siku zao.
Anasema kuwa wafuasi wake wanafahamu sheria ile. Japo wanakutana mara moja kwa mwaka, kunayo nafasi ya wao kufika pale Jumamosi kuzungumza na Mungu wao.
“Jumamosi usiku hutakosa watu hapa. Wengi wao hutenga muda wao wa kuabudu. Lakini hii sehemu takatifu ambayo haihitaji watu wachafu. Na wanajua hilo,” anasema.
Katika sehemu hiyo, kuna mti wa mugumo na pande za kushoto na kulia, kuna nyumba kila upande maalum kwa wafuasi wale.
“Upande huu wa kushoto kuna nyumba inayotumiwa na wasichana na akina mama na pande wa kulia ni nyumba ambayo hutumiwa na wanaume wa umri wote. Wakati mwingine wanapolazimika kulala huku, wao hutumia nyumba hizo,” akasema.
Lakini waumini hao hawatumii Biblia, licha ya kusikika wakinukuu maandiko ya kitabu kitakatifu. Taifa Jumapili ilipouliza kuhusu suala hilo, bila shaka ilipewa jibu.
“Kile ninajua ni kwamba Mungu wetu bado yuko. Huyo Mungu ndiye aliumba Mumbi na Agikuyu. Sisi tulikuwa tunapokea ujumbe au kufahamu ujumbe huo kutokana na majira,” akafichua Bi Wahu.