Chifu adai polisi wanahujumu vita dhidi ya pombe haramu
MAAFISA wa serikali katika baadhi ya maeneo sasa wanahujumiana katika vita dhidi ya pombe haramu, imefichuka.
Chifu wa Riruta Bw Joseph Murage aliambia Taifa Jumapili kwamba baadhi ya polisi huungana na kuchochea raia kuwashambulia maafisa wa utawala ambao hutekeleza msako wa kumwanga pombe haramu na kuwakamata wauzaji na walevi.
Bw Murage alisema machifu wamejitolea kikamilifu kutii amri kutoka kwa afisi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, lakini sasa baadhi ya polisi ni kikwazo.
“Niliambiwa pombe ikipatikana hapa nitaikunywa yote… Inasikitisha siwezi nikawashughulikia walevi na wauzaji wa pombe kwa sababu nimewekewa kizingiti,” alisema Bw Murage.
“Kuna mahali ambapo tulishambuliwa kwa mawe na raia mchana. Baadaye tuligundua wapo polisi ambao walipanga tupigwe. Tulishindwa kwa nini tunapigwa na tuko na gari aina ya landcruiser ambalo tulipewa na polisi wakati wa msako,” akasema.
“Walitupiga wakipiga kelele kwamba tunaharibu chakula. Eti, busaa ni chakula,” akaongeza.
Alidai maafisa waliokuwa pamoja nao kutekeleza msako walikuwa na mienendo isiyoeleweka.
“Tulikuwa tunaona mmoja mmoja ananunua maji na airtime kutoka kwa duka. Kiufupi tuliachwa peke yetu,” akasikitika.
Kiongozi huyo amewataka wakazi wa Kaunti ya Nairobi kuunga machifu mkono wanapokabiliana na pombe haramu ambayo inazidi kuwaangamiza vijana.
Alilamikia kile alidai ni polisi kujikokota kuwakamata wauzaji pombe licha ya ripoti kupigwa.
“Ni upuzi mtupu mwananchi kupiga ripoti kuwa pombe haramu inauzwa, lakini ukifahamisha polisi unaambiwa kuwa hakuna gari la kuwaleta kumshika mhalifu,” aliongeza.
Pia, aliwataka wamiliki wa nyumba za wapangaji kuwa macho na kujua mtu anafanya biashara gani katika nyumba.
“Wamiliki wa nyumba ndio hawataki kuwatoa. Niliongelesha mwingine kwa njia ya barua amuondoe mhalifu tuliyemshuku lakini akapuuza,” alisema chifu huyo.
Msimamizi wa kituo cha polisi cha Riruta Sarah Kimsar alipinga madai yaliyotolewa na Bw Murage kuwa polisi wa kituo chake walipanga njama na wananchi kuwarushia mawe.
Bi Kimsar, pia alisema wako katika nafasi ya kwanza kuhakikisha pombe hiyo haramu haipatikani eneo lake.
“Nimekuwa nikiongea na vijana wa eneo hili kuepuka unywaji pombe haramu. Maafisa wangu wana jukumu la kuhakikisha pombe hiyo inatokomezwa,” akasema Bi Kimsar.
Ingawa madai mengine yaliibuka kwamba kuna hujuma baina ya polisi wa kawaida na wale wa utawala na kwamba hilo huenda pengine linachangia vita dhidi ya pombe kutozaa matunda.
Mwezi Februari 2024, Bw Gachagua alieleza jinsi afisi yake inakumbwa na changamoto katika vita dhidi ya pombe haramu lakini akasema atafanikiwa kivyovyote vile bila kuogopa kupoteza kura za walevi.