Habari za Kitaifa

Mwaura alaani mauaji ya mwanablogu 

March 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA ALEX NJERU

SERIKALI imelaani mauaji ya mwanablogu wa Tharaka Nithi Peris Mugera ambaye mwili wake ulipatikana umetupwa katika kaunti ya Kirinyaga.

Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura kauli tofauti zinazotolewa kupitia majukwaa mbadala ya habari haziwezi kuzimwa.

Bi Mugera, ambaye pia alikuwa mfanyabiashara, alikuwa buheri wa afya alipoondoka katika nyumba yake ya kukodisha mjini Chuka kaunti ya Tharaka Nithi Alhamisi wiki jana kulingana na watoto wake wawili wenye umri wa miaka sita na 15.

Inasemekana kuwa Mugera, 40, ambaye hayuko kwenye ndoa, aliwaambia mabinti zake kwamba angekutana na rafiki mmoja kisha aelekee kazini kwingineko kisha arejee nyumbani jioni.

Hata hivyo, mama huyo hakufahamu kuwa hayo ndio yalikuwa mazungumzo yake ya mwisho na watoto wake.Kwenye ujumbe wake wa mwisho katika ukurasa wake wa Facebook mnamo Februari 25, saa tisa na dakika nne alasiri, Mugera alilalamika kuwa mwili wake unahitaji tiba.

“Mwili wangu unauma. Nani anaweza kunisaidia dawa,” sehemu ya ujumbe wake ikasema.

Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Tharaka Nithi Wesley Koech, mwili wa Mugera ulipatikana kando ya Makutano-Sagana katika kaunti ya Kirinyaga Jumatatu.

Hata hivyo, hakutambuliwa mara moja.

Maiti hiyo ilitambuliwa Ijumaa na jamaa na marafiki zake na maafisa wa polisi baada ya picha yake kusambazwa katika mitandao ya kijamii.

“Kuna uwezekano mkubwa kuwa Mugera aliuawa kati wakati aliondoka nyumba na Jumatatu asubuhi wakati maiti yake ilipatikana na wapiti njia kando mwa barabara,” akasema Bw Koech.

Habari kuhusu kupotea kwa mtu iliwasilishwa katika kituo cha Polisi cha Chuka mnamo Machi 1 na jamaa za Mugera na uchunguzi ukaanzishwa mara moja.Hii ni baada ya watoto wake kumpasha habari mmiliki wa nyumba yao Jumamosi jioni ambaye aliwapasha habari marafiki za Mugera baada ya kufeli kumfikia kwa njia ya simu.

Kulingana na polisi, mawimbi ya siku yake ya mkononi yalirekodiwa mara ya mwisho saa nane alasiri Ijumaa katika Kathoge, Kirinyaga na tangu wakati huo haikuwa imewashwa.Kisa hicho cha mauaji kiliripotiwa katika kituo kidogo cha polisi cha Rukanga katika Kaunti Ndogo ya Mwea.

Maafisa hao wakiongozwa Afisa Msimamizi wa Kituo cha Polisi (OCS) na wale wa Idara ya Upelelezi wa Janai (DCI) walifika eneo la tukio na kupata mwili huo ukiwa na majeraha kichwani.

Kulingana na Bw Koech, mauaji ya Mugera sio kisa cha kila mara na kwamba maafisa wa polisi wanaendeleza uchunguzi kwa lengo la kuwanasa wahusika na kuwafikisha mahakamani.