• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Pogba, De Gea na Lukaku walichochea kufutwa kwangu – Mourinho

Pogba, De Gea na Lukaku walichochea kufutwa kwangu – Mourinho

LONDON, UINGEREZA

PUNDE baada ya kupigwa kalamu na Manchester United Jumanne asubuhi, mkufunzi maarufu wa klabu hiyo, Jose Mourinho aliandaa kikao na kutoa kilio chake huku akimlaumu sana kiungo wake Paul Pogba.

Jose alitimuliwa na klabu hiyo kufuatia matokeo mabaya zaidi ya klabu hiyo hasa baada ya Manchester United kutandikwa na mahasimu wao wa tangu jadi Liverpool mabao 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza mnamo Jumapili uwanjani Anfield. Manchester United inashikilia nafasi ya sita ligini kwa alama 26 pekee kutokana na mechi 17. Inashindwa na viongozi Liverpool kwa alama 19.

Siku chache zilizopita Mourinho almaarufu The Special One alikuwa amemtaja Pogba kama kirusi (kinachoharibu timu yake). Mourinho, aliyemnunua Pogba kutoka Juventus kwa zaidi ya Sh15 bilioni, alikuwa akimweka kwenye benchi mwanasoka huyo katika mechi za hivi karibuni.

“Pogba anapenda kuonyesha miondoko yake ya kucheza densi kwenye instagram kuliko kucheza vizuri uwanjani,” alisema Mourinho baada ya kuonyeshwa paa. Pia kocha huyo aliyewahi kufundisha Chelsea, Inter Milan, Real Madrid na Porto aliwakashifu wanasoka wengine wa kikosi hicho akiwemo Romelu Lukaku na kipa David de Gea kama walioishiwa maarifa.

Mourinho, 55 anamwaga unga miezi 11 tu baada ya Manchester United kuongeza kandarasi yake hadi mwaka 2020. Ripoti zinadai klabu hiyo itamfidia Sh3.1 bilioni kwa kumpiga teke mapema.

Presha imekuwa ikiongezeka kwa Mourinho tangu alipoanza kukosana na kiungo Pogba msimu uliopita.

Kichapo cha uwanjani Anfield kilithibitisha mwanzo mbaya kabisa wa United ligini katika kipindi cha miaka 28.

Inasemekana kwamba Mourinho alilia alipokosa kuteuliwa kujaza nafasi ya Sir Alex Ferguson alipostaafu mwisho wa msimu 2012-2013 kama kocha wa United. David Moyes alipewa kazi hiyo msimu wa 2013-2014, lakini akatimuliwa kabla ya msimu huo kutamatika. Ryan Giggs alishikilia nafasi hiyo kwa muda kabla ya majukumu hayo kupokezwa Mholanzi Louis van Gaal, ambaye alikuwa usukanini kutoka Mei mwaka 2014 hadi Mei 23, 2016.

Mourinho aliajiriwa na United mnamo Mei 27, 2016 kwa kandarasi ya miaka mitatu. Miaka mitano tangu alie alipokosa kuchaguliwa kuwa mrithi wa Ferguson, baada ya kupata kazi ya kunoa klabu aliyoitamani sana, enzi yake ilifikia kikomo kwa machozi.

Aidha, ripoti nchini Ufaransa zinadai Zinedine Zidane “atapenda” kuchukua nafasi ya Mourinho, ambaye kwa mara ya kwanza ameondoka klabuni bila kushinda ligi, tangu mwaka 2002. Katika msimu wake wa kwanza uwanjani Old Trafford, Mourinho alishinda mataji ya Europa League na FA. Msimu jana alimaliza wa pili ligini.

Tetesi zinasema nyota wa zamani wa United, Mochael Carrick ameteuliwa kushikilia majukumu yaliyofanywa na ‘Special One’ kwa siku mbili zijazo, klabu hiyo ikitafuta kocha wa muda kutoka nje.

Ripoti zinasema kwamba kocha mpya kutoka nje ataongoza United hadi msimu huu wa 2018-2019 utamatike. Mchezaji wa zamani wa United, Ole Gunnar Solskjaer, ambaye anafundisha klabu ya Molde nchini mwake Norway, amehusishwa na kazi hii ya kunoa United hadi mwisho wa msimu huu. Katika kikao chake cha mwisho na wanahabari kilichokuwa baada ya Liverpool kupoteza, Mourinho alilaumu wachezaji kadhaa wakiwemo kiungo Paul Pogba, mshambuliaji Romelu Lukaku na kipa David De Gea kwa masaibu yake.

You can share this post!

Mfumo mpya wa ugavi wa fedha za kaunti

Bunge lamwidhidnisha Mbarak kuwa CEO wa EACC

adminleo