Maafisa waliohudumu zaidi ya miaka 3 kwenye kituo Mlima Kenya waanza kuhama
NA MWANGI MUIRURI
MAAFISA wa polisi ambao wamehudumu Mlima Kenya kwa zaidi ya miaka mitatu wameanza kuhamishwa kupitia amri ya Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki.
Kikatiba, maafisa wa polisi huhamishwa kupitia majadiliano ya tume ya huduma ya kikosi cha polisi (NPSC) na idara hiyo inayoongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi, kwa sasa akiwa ni Bw Japhet Koome.
Prof Kindiki akiwa Mjini Murang’a Machi 8, 2024 alisema kwamba kabla ya jua kutua siku hiyo alitarajia wote ambao wataathirika na amri hiyo wawe wamefahamishwa watakaporipoti kazi kesho yake.
“Na hakuna cha kutoa vijisababu. Ukiwa umehudumu katika stesheni uliyo kwa zaidi ya miaka mitatu, hakuna haja uamkie kazi hapo kesho. Uulize umetumwa wapi ikiwa hautakuwa umepata barua,” akasema.
Alisema kwamba miongoni mwa maafisa hao ambao wamehudumia stesheni moja kwa muda mrefu ndio huibuka watundu, mang’aa na wakora ambao huhujumu sera za utekelezaji sheria.
Akiwa katika ziara za Kaunti za Kiambu, Murang’a, Kirinyaga na Nyeri, Prof Kindiki alisema maafisa hao wakikaa katika eneo moja kwa muda mrefu ndio huingiwa hata na bongo la biashara na kuanza kukimbizana na mitandao ya magendo.
Alisema kero ya ulevi kiholela na upenyo wa mihadarati nchini unahusikana moja kwa moja na utundu wa baadhi ya maafisa wa kiusalama.
“Kwa sasa hatuna mchezo na ni lazima maafisa wa serikali wafanye kazi ambayo waliajiriwa kutekeleza la sivyo waondoke. Kuhusu kero ya ulevi na mihadarati, hatuna nafasi ya wanasiasa kwa kuwa ni msako wa kiusalama kudhibiti maafa, umaskini na magonjwa. Wanasiasa sasa wakae mbali na vitengo vya kiusalama,” akasema.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kumekuwa na mvutano wa ubabe wa kisiasa baadhi ya wanaowania usemaji wa mlimani ndani ya serikali wakipinga kuhamishwa kwa baadhi ya maafisa ndani au nje ya eneo hilo.
Maafisa wengi wamejipata wakitumwa kuhudumu eneo hilo lakini wakapingwa huku wengine wakihamishiwa kwingine lakini misukumo ya kisiasa ikiwafanya kubakia katika stesheni zao.
Aidha, kumekuwa na visa vya wanasiasa kuvamia vituo vya polisi na kuwatimua maafisa wa polisi kutokana na madai ya ufisadi, uzembe au utepetevu.
Prof Kindiki alisema kwamba hali hizo zote zimefika kikomo na hakutakuwa na mwingilio wa kisiasa akisisitiza kwamba wote katika utekelezaji sheria wataafikia yanayowahusu kwa mujibu wa sheria.
Prof Kindiki alishikilia kwamba hakuna afisa wa polisi ambaye ana ruhusa ya kuwekeza katika biashara ya baa.
“Ni aidha uwe mwekezaji wa baa au uwe afisa wa polisi. Hakuna cha kuunganisha kazi hizo mbili. Pia, maafisa kulewa kiholela tumekataa na tutakuwa macho sana kuwamulika walevi kikosini.
“Huwezi ukatumwa kazi ya kupambana na ulevi ukiwa mlevi. Hautatumwa kupigana na mihadarati ukiwa wewe ni mraibu,” akasema.
Waziri Kindiki alisema kwamba kikosi cha usalama ni lazima kizingatie nidhamu na uadilifu pamoja na utiifu na uzalendo.