Afueni kwa wakulima mbolea nafuu ikitua nchini
NA BARNABAS BII AND STANLEY KIMUGE
WAKULIMA katika maeneo yanayokuza mahindi wamepata afueni baada ya serikali kuagizia kutoka nje magunia 12.5 milioni ya mbolea itakayotumika msimu huu wa upanzi.
Waziri wa Kilimo Mithika Linturi amesema tani kadhaa za shehena hiyo zimewasilishwa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Nchini (NCPB) eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa ili kukidhi mahitaji ya wakulima.
Mbolea hiyo ya bei nafuu inayouzwa kwa Sh2,500, inapatikana kwenye mabohari ya NCPB mijini Eldoret, Kitale, na kwingineko eneo hilo.
“Tulikamilisha zabuni Desemba na ninataka kuwaeleza wasambazaji bidhaaa kuwa hatutaruhusu uzembe, hatutakubali watakaokosa kutimiza kwa wakati ufaao. Nimewaagiza kunipa ripoti yao kufikia Jumatatu (Machi 11, 2024),” alisema Waziri alipohudhuria Maonyesho ya Kilimo (ASK) Eldoret, Ijumaa.
“Tumepokea malalamishi kutoka kwa wakulima na tunayashughulikia. Tumegundua kumekuwa na ongezeko la matumizi ya vifaa vya kilimu msimu huu ikilinganishwa na msimu uliopita.”
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Utafiti kuhusu Kilimo na Mifugo Nchini (KARLO) inaashiria kwamba kuendelea kutumia mbolea ya kawaida kunawasababishia wakulima katika kaunti za Uasin Gishu na Trans-Nzoia kupoteza jumla ya mifuko 10 ya mahindi kila msimu wa kuvuna kutokana na kudorora kwa rotuba ya udongo.
Wakulima wengi hawajui aina ya udongo wanaotumia ili kujua mbolea wanayopaswa kukuzia mimea yao.
Inawagharimu wakulima kati ya Sh1,500 na Sh2,000 kuchukua chembechembe za udongo wao ili kupima kiwango cha asidi na alikali katika udongo wao.