Habari za Kaunti

Uzinduzi wa vitabu vya Kibajuni kudumisha tamaduni  

March 11th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

HISTORIA imeandikishwa baada ya vitabu vilivyoandikwa na kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwa lahaja au lugha ya Kibajuni kuzinduliwa rasmi kisiwani Lamu mwishoni mwa juma.

Vitabu hivyo ni pamoja na ‘Chusomeni Kibajuni’ kinacholenga wanafunzi wa Shule za Msingi, hasa wale wa Gredi 1, 2 na 3.

Waandishi wa kitabu hicho ni Yumna Hamid Titi kwa ushirikiano na Fuad Aroi na Yumbe Athman.

Kitabu hicho kinatarajiwa kuwezesha wanafunzi kujua kwa undani zaidi Kibajuni, kukiongea na pia kukiandika, hivyo kukikuza na kukiendeleza.

Vitabu vingine vilivyozinduliwa kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Mwana Arafa mjini Lamu ni ‘Mashairi ya Kibajuni’ ambao ni mkusanyiko wa zaidi ya mashairi 100 yenye asili ya Kibajuni yaliyohakikiwa na Omar Lali na Omar Maulana, ‘Shivulani ni Shaulani,’ ambacho pia ni kitabu cha mkusanyiko wa mashairi ya mbinu ya kutamka au kunena yaliyotayarishwa na mshairi mneni, Mohamed Kombo.

Pia kuna kitabu kingine cha mkusanyiko wa machapisho ya Kibajuni ambacho kilihakikiwa na Prof Kimani Njogu na Athman Lali Omar.

Vitabu vyote vilivyozinduliwa vya Kibajuni pia vinaandamana na miongozo yake ya kuwaelekeza na kuwafafanulia zaidi wanafunzi, hivyo kuwawezesha kuelewa yaliyomo na kuhakikisha wasomi hao wanajipatia maarifa kulingana na Mtaala wa sasa wa Elimu nchini (CBC).

Uzinduzi wa vitabu hivyo umetekelezwa kupitia Mradi wa Kuhifadhi turathi, hasa zile za lugha ya Kibajuni ili kusaidia kizazi cha sasa na kijacho kujua na kujifunza lugha hiyo ili isiangamie siku zijazo.

Mradi wa kuitafiti na kunakili lahaja ya Kibajuni unatelekezwa kupitia Shirika la Twaweza Communications Center kwa ushirikiano na lile la Shungwaya Welfare Association na Swahili Resource Centre.

Mradi huo unafadhiliwa na Baraza la Uingereza Linalolinda Tamaduni likishirikiana na Idara ya Utamaduni Kidijitali, Mawasiliano na Michezo.

Ni mara ya kwanza kwa lugha ya Kibajuni, ambayo lahaja yake inalinganishwa na Kiswahili kuweza kupata uchapishaji rasmi wa vitabu kama hivyo.

Wadau mbalimbali na wazee wa jamii ya Wabajuni wakionyesha vitabu vilivyochapishwa kwa lugha asili ya Kibajuni. PICHA|KALUME KAZUNGU

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa vitabu hivyo, Msimamizi wa Shirika la Twaweza Communications, Prof Kimani Njogu alisema mradi huo wa kurekodi lahaja ya Kibajuni na kuichapisha utasaidia pakubwa kuikinga lugha hiyo isipotee.

Pia itasaidia kutambua mambo mengine mapya zaidi yanayofungamana na Kibajuni.

“Kuijua lahaja ya Kibajuni na kuienzi ni jambo mwafaka litakalosaidia kuifahamu zaidi jamii ya Wabajuni na historia yake. Pia ni mbinu ya kuhifadhi historia na ukale wa Wabajuni, hivyo kusaidia kizazi kijacho,” akasema Prof Njogu.

Kumekuwa na malalamishi na majadiliano kwamba endapo lahaja ya Kibajuni itaendelea kutofundishwa shuleni, vijana wengi wa asili ya Wabajuni watapotoka, hivyo kukosa uwezo wa kuizungumza au kuiandika lahaja hiyo.

Katibu Mkuu wa muungano wa Shungwaya Welfare Association, Omar Lali aliwapa changamoto vijana wa asili ya Kibajuni kuienzi lugha yao na kuitumia kwenye mazungumzo ya kila siku bila kujihisi kuwa dhaifu.

“Ningesihi vijana kujivunia lugha yao ya Kibajuni. Lugha huashiria kikamilifu historia ya jamii au watu fulani. Ni raslimali muhimu ya utamaduni,” akasema Bw Lali.

Mradi huo pia unaendana na matakwa yaliyomo kwenye Katiba ya Kenya inayotambua umuhimu wa lugha ya watu wa Kenya.

Akizungumza kwenye hafla hiyo ya uzinduzi wa vitabu vya Kibajuni, Afisa Mshauri wa Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Bw Nagaoka Masanori, alitaja uzinduzi wa vitabu hivyo vya Kibajuni kuwa mwafaka katika kuhifadhi ukale na tamaduni za watu wa Lamu ambao ni Waswahili wa asili ya Wabajuni.

Ikumbukwe kuwa Lamu ni miongoni mwa maeneo machache ulimwenguni yaliyoorodheshwa na UNESCO mnamo 2001 kuwa sehemu zinazotambulika kwa kuenzi, kuhifadhi na kuendeleza ukale wake-yaani Unesco World Heritage Site.

“Uzinduzi huu ni muhimu kwa historia, uhifadhi na uendelezaji wa tamaduni na mila za Lamu ambao ni mji wa kipekee ulimwenguni kutokana na jinsi unavyoenzi ukale,” akasema Bw Masanori.

Wengine waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa vitabu vya lugha ya Kibajuni ni Mkurugenzi wa Baraza la Uingereza Kenya na Mshirikishi Mkuu wa Ukanda wa Afrika Mashariki, Bw Tom Porter, Naibu Mkurugenzi wa Tume ya Kitaifa ya Kenya katika UNESCO, Bi Emily Njeru, wawakilishi wa serikali ya Kaunti ya Lamu, na jamii, ikiwemo wazee.