Makala

Sababu ya korti kumruhusu Kibor kumtaliki mke wa tatu

December 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na TITUS OMINDE

MKULIMA na mfanyabiashara maarufu kutoka Kaunti ya Uasin Gishu Mzee Jackson Kibor jana alisema sasa atafurahia maisha yake ya uzeeni baada ya mahakama ya Eldoret kumruhusu amtaliki mke wake wa tatu.

“Leo hii nina furaha nyingi baada ya kufaulu kumtaliki mke wangu wa tatu, nitalala usingizi mnono na mke wangu mdogo. Nitaishi kwa miaka mingi,” alisema Mzee Kibor mwenye umri wa miaka 85.

Mahakama iliidhinisha kuachana kwa wanandoa hao baada ya Kibor kuwasilisha mahakamani kesi nambari 22 ya mwaka wa 2018 akidhamiria kumtaliki mke wake wa tatu.

Hii inatokea baada ya Mzee Kibor kufaulu kumtaliki mke wake wa pili mnamo Oktoba mwaka jana.

Mzee Kibor alionyesha furaha isiyo na kifani baada ya mahakama kukubali ombi lake la kumtaliki mke wake wa ndoa ya miaka 43, Bi Naomi Jeptoo Kibor.

Kigezo kikuu ambacho Mzee Kibor alizingatia katika talaka yake ni madai kwamba mke wake alimuacha na kuhama kutoka katika ndoa yao pamoja na watoto wake sita.

Mlalamishi huyo alidai kuwa mke wake alibadili tabia baada ya kuondoka katika ndoa yao ambapo amekuwa akimuonyesha uhasama na uadui mbali na kumpuuza kila mara.

Hakimu mwandamizi wa Eldoret, Bi Naomi Wairimu alitoa idhini kwa mzee Kibor kumtaliki mke wake kwa kuzingatia madai ambayo yanaoana na madai yaliyotumika kuidhinisha talaka dhidi ya mke wa ndoa ya pili katika ndoa ya miaka 52 mwaka jana katika mahakama ya hakimu mkuu wa Eldoret.

Kupitia kwa wakili wake Bw Stanley Kagunza Kibor, Bw Kibor alidai kuwa Jeptoo amekuwa na mazoea ya kumnyima tendo la ndoa mbali na kuchochea watoto wake kumkosea heshima na kumuonyesha uhasama.

“Nina furaha siku ya leo baada ya uamuzi huu. Mke wangu amekuwa akinionyesha uhasama wa hali ya juu, jambo ambalo liliniathiri kisaikolojia. Kwa sasa naweza sema kwa ujasiri kuwa nitaishi kwa miaka mingi zaidi,” alisema Kibor huku akionyesha tabasamu kuu.

Hata hivyo, madai yake yalikataliwa na mshtakiwa ambaye alitilia mkazo kwamba anampenda mume wake huku akiambia mahakama kuwa ndoa yao imejaa upendo.

“Hii talaka haina msingi. Kile ninachojua ni kwamba ninampenda mzee wangu pamoja na watoto wetu sita, sioni ni kwa nini mahakama imeidhinisha talaka hii,” alisema Bi Jeptoo.

Kwa upande wake, Mzee Kibor alisema ndoa baina yao iligonga ukuta na haingerekebika kwa njia yoyote ile.

Bw Kibor aliambia mahakama kuwa juhudi za familia za pande zote mbili kupatanisha wawili hao ziligonga mwamba. Kibor ambaye ana wake wanne alioa mke huyo wa tatu mwaka wa 1975 chini ya sheria za kitamaduni za jamii ya Wanandi.

Mmoja wa wake hao wanne ni marehemu. Mke mdogo wa Kibor, Bi Yunita Kibor mwenye umri wa miaka 37 aliolewa na mzee huyo mwaka wa 2002.

Akitoa hukumu yake hapo jana, hakimu Wairimu alisema baada ya kuzingatia utetezi kutoka pande zote, ni bayana kuwa mahakama haikuwa na uwezo wa kudumisha ndoa hiyo.

Bi Kibor ana siku 14 kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo wa mahakama.