Habari za Kaunti

Utata wa soko la Kombani wachacha

March 11th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

WAKAZI wa kaunti ya Kwale watasubiri kwa wiki mbili zaidi kufahamu iwapo soko la Kombani lililogarimu Sh120 milioni litafunguliwa kuona ikiwa litawafaa wakulima na wafanyabiashara 7,000 au la.

Hii ni baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kuhusu kufunguliwa kwa soko hilo kusongeshwa mbele huku wanakandarasi na kaunti wakizozana mahakamani.

Maamuzi ambayo yaliratibiwa kutolewa Machi 8, imesogezwa mbele kwa wiki mbili zaidi.

“Nimeagizwa kuwajulisha kuwa hukumu ya rufaa hii iliyokuwa itolewe leo Machi 8, imesongeshwa mbele hadi Machi 22,” barua pepe iliyotumwa kwa wahusika katika kesi hiyo ilisema

Hii ni mara ya tano kwa Mahakama ya Rufani kuahirisha hukumu hiyo kwani uamuzi umekosa kutolewa mara nne kutokea Desemba 8, 2024.

Uamuzi huo ulisongeshwa hadi Februari 8, kisha Februari 23, Machi 8, na sasa Machi 22.

Kesi hiyo inahusu mgogoro kati ya kaunti na mkandarasi wa kampuni ya End to End Limited kuhusu zabuni ya ujenzi wa Soko la Kombani.

Kampuni hiyo ya ujenzi imepinga kufunguliwa kwa soko hilo ikidai kuwa kaunti ilikiuka mkataba wao na kuisababisha kupata hasara kubwa.

Pia inataka kulipwa fidia kutokana na kuvunjika kwa mkataba huo.

Kampuni hiyo ilishtaki kaunti na kupata agizo la mahakama kuzuia shughuli zozote zisifanyike sokoni hadi lalama zake zishughulikiwe.

Mwanakandarasi huyo anadai malipo ya Sh44 milioni kati ya jumla ya Sh106 milioni zilizowekezwa kujenga soko hilo.

Soko hilo lililo karibu na makutano ya barabara kuu ya Mombasa-Lunga-Lunga-Tanzania na Kwale-Kinango huko Matuga lilifunguliwa tena Oktoba 10, 2022, licha ya kesi zinazoendelea mahakamani.

Hili lilipelekea kampuni hiyo kwenda katika Mahakama Kuu ya Mombasa siku tatu baadaye, kutafuta maagizo zaidi ya kuzuia gatuzi hiyo kuruhusu shuguli za uuzaji kufanyika katika soko hilo.

Jaji wa Mahakama Kuu Njoki Mwangi alikubali ombi la kampuni hiyo na kutoa maagizo mnamo Oktoba 25, akipiga marufuku kufunguliwa, kuzindua au kuingia katika soko hiyo hadi mzozo huo utatuliwe.

Serikali ya kaunti hiyo ilikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa mnamo Desemba 2, 2022, ikitaka maagizo ya Jaji Mwangi kutupiliwa mbali.

Soko la jumla la mazao ya Kombani limefungwa kutokana na kesi hii. Ujenzi wake ulikamilika miaka mitatu iliyopita.

Aidha, lilipaswa kufunguliwa Desemba 2021 ili kusaidia wakulima na wafanyabiashara zaidi lakini mzozo huo umesimamisha kila kitu.