Mtandao wa wezi wanaolenga ng’ombe wa maziwa
NA MWANGI MUIRURI
WAFUGAJI eneo la Mlima Kenya waNAteta kuhusu ongezeko la wizi wa mifugo hasa ule unaolenga ng’ombe wa maziwa.
Wanalalamika kwamba serikali imezembea kwa kiwango kiku, sekta ya maziwa ikiathirika kwa kiwango kikubwa.
Suala hilo likiendelea kufumbiwa macho licha ya malalamishi kuibuka, wahuni wanaiba ng’ombe wanaozalisha maziwa pamoja na ndama wao.
“Wakulima wanakadiria hasara kubwa kuibwa anayetoa maziwa na ndama wake,” akasema mwenyekiti wa muungano wa wafugaji wa kibiashara ukanda wa kati, Bw Stephen Mwaura.
Kando na ng’ombe, mtandao wa wahuni umeanza kuvamia mifugo wengine kama vile kuku, mbuzi, nguruwe na sungura.
Bw Mwaura alisema wizi huo umepunguza biashara ya bidhaa za mifugo eneo hilo kwa asilimia 60 sasa.
“Ni hujuma kuu ya kiuchumi mashinani na hatutakuwa na uwezo kushiriki biashara ya bidhaa za mifugo. Hatutaweza kujenga uchumi kwa manufaa yetu na ya nchi kwa kuwa wezi wataiba,” akalia.
Alisema kwamba kwa sasa Mlima Kenya imeandamwa na utepetevu miongoni mwa vyombo vya usalama ambapo hata baada ya wafugaji kulalamika mara kwa mara, uovu huo hauzimwi.
Bw Mwaura alisema wakulima ambao wamechoka kungoja afueni ya serikali, wamekuwa wakichukua sheria mikononi kupitia kuchoma washukiwa, wengine wakitafuta afueni za kiuchawi.
Hata hivyo, Kamanda wa polisi eneo la Kati Bi Lydia Ligami alisema kwamba kwa sasa serikali inajizatiti kupambana na wezi wa mifugo.
Afisa huyo anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo.
“Shida hiyo ipo mashinani. Tumejikaza kukabiliana na hali hiyo kwa uwezo wetu wote tukishirikiana na jamii za eneo hili,” akasema.
Alisema kwamba kila kituo cha polisi eneo hilo kimepewa amri ya kukabiliana na kero hiyo kwa kila mbinu iliyoko katika sheria.
Lakini Bw Mwaura aliteta kwamba polisi wanasema wapepunguza visa hivyo lakini sio kwa sababu ya mikakati ya kiusalama, bali ni kwa kuwa mifugo wameibwa kiasi kwamba hakuna tena wengi wa kulengwa na wezi.
“Wizi unapungua kwa kuwa wakulima hawafugi tena. Sio kwa sababu eti polisi wamefanya kazi,” akasema.
Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alisema kwamba wizi wa mifugo eneo hilo huwakilisha asilimia 70 ya visa vya uhalifu kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Hii ina maana kwamba sekta za maziwa, nyama, mayai na ngozi pamoja na uuzaji wa wanyama zimesambaratika. Tunafaa tutafute mbinu ya kumaliza wizi huu ili tufungue mianya ya kuinua jamii zetu kiuchumi,” akasisitiza.
Alisema hiyo ndiyo sababu eneo la Mlima Kenya hukosa viwanda dhabiti vya sekta ya ufugaji, huku bei ya nyama ikipanda kiholela kutokana na uhaba wa mifugo wa kuchinjwa.
“Bila ng’ombe ina maana kuwa hakuna maziwa,” akasema mwenyekiti wa umoja wa wafugaji na biashara husika Bw Martin Kamande.
Mbunge mwakilishi wa Kaunti ya Kirinyaga Bi Njeri Maina aliteta kwamba hata wakulima wanaotegemea ng’ombe na punda katika sekta ya uchukuzi wameumia.
“Kama kwetu Kirinyaga kuna ng’ombe ambao hutumika kuvuta mashine za kulima shamba. Wachuuzi wa maji wanategemea ng’ombe hao pamoja na punda. Wezi wa mifugo wanavamia maboma na kuiba mifugo, hivyo basi kuhangaisha wanaotegemea mifugo kujiendeleza kimaisha,” akasema.
Bi Maina aliitaka idara ya usalama ijue kwamba wizi huo umegeuka kuwa janga la kiuchumi.