Kampuni 19 zapata ruhusa ya CBK kutuma maelezo ya wakopaji CRB
NA WANDERI KAMAU
BENKI Kuu ya Kenya (CBK) Jumatatu ilitoa leseni kwa kampuni 19 zaidi za kutoa mikopo kidijitali kupitia simu, hilo likifikisha idadi ya kampuni hizo kuwa 51 nchini.
Hali hiyo pia imetajwa kuchangiwa na idadi kubwa ya Wakenya wanaokimbilia kuchukua mikopo midogomidogo kupitia simu kukidhi mahitaji yao, kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha.
Kufikia sasa, kuna zaidi ya kampuni 400 za kutoa mikopo hiyo ambazo zimetuma maombi ya kupata leseni kutoka kwa CBK.
Wakenya wengi wanasema wamekuwa wakikimbilia kuchukua mikopo kutoka kwa kampuni hizo, kwani huwa hazina masharti mengi ikilinganishwa na benki.
Kwa sasa, kuna jumla ya benki 39 nchini.
Wawekezaji wengi wamekuwa wakiegemea biashara hiyo, kutokana na idadi kubwa ya Wakenya wanaotafuta mikopo hiyo.
Kwa mfano, mnamo Februari 2023, kampuni ya Tala ilitangaza ilikuwa imetoa mikopo ya hadi kiwango cha Sh272 bilioni.
Ikizingatiwa Tala imekuwa ikihudumu nchini kwa karibu miaka tisa, hilo linamaanisha kwamba imekuwa ikitoa mikopo ya Sh32.2 bilioni kila mwaka.
CBK inasema imepokea maombi 480 tangu Machi 2022, ila imekuwa ikishirikiana na wawekezaji hao, kwa kuwafahamisha kuhusu masharti wanayofaa kuzingatia kabla ya kupewa kibali.
Kwenye mchakato wa kutoa leseni, CBK pia imekuwa ikishirikiana na taasi kama vile Afisi ya Kamishna wa Kulinda Data.
Baadhi ya kampuni zilizopewa leseni za kuhudumu ni Lipa Later Limited, Ceres Tech, Azura Credit, Chapeo Capital, Chime Capital, Creditarea Capital, Decimal Capital, Dexintec Kenya Limited, Factorhouse Limited na Fezotech Kenya Limited.
Nyingine ni Fortune Credit Limited, Lobelitec Credit, Maralal Ledger, Marble Capital Solutions, MKM Capital, Pi Capital Limited, Senti Capital, UbaPesa Limited, na Zillions Credit Limited.
Kutokana na hatua hiyo, hilo linamaanisha kwamba kampuni hizo zitakuwa na ruhusa ya kutuma majina ya watu watakaoshindwa kulipa mikopo hiyo kwa Mamlaka za Kudhibiti Mikopo (CRB).