Bambika

Alikiba afungua kituo cha redio na televisheni

March 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

BAADA ya kuwa kwenye tasnia ya burudani kwa miongo miwili, mwanamuziki Alikiba kutoka Tanzania ameamua kufuata nyayo za msanii mwenzake, Diamond Platnumz, kwa kufungua kituo cha redio na televisheni kwa wakati mmoja.

Kwa muda mrefu, Diamond ndiye amekuwa akitkisa tasnia ya burudani nchini humo, baada ya kuzindua kituo cha redio na televisheni cha Wasafi FM na  Wasafi TV mtawalia mnamo 2022.

Katika hatua iliyoonekana kama njia ya kumwiga mshimdani wake wa muda mrefu Diamond, Alikiba alitangaza kuzindua kituo cha redio na televisheni cha Crown FM na TV Jumamosi, Machi 10, 2023, kama njia ya “kuwashukuru mashabiki wake”.

Kampuni hiyo inaitwa Crown Media na itajumuisha kituo cha redio na televisheni pamoja na huduma za masuala ya kidijitali na upangaji hafla.

Kwenye hafla hiyo ya kufana, King Kiba alisema kuwa wakati wa “kuchukua mkondo tofauti wa burudani”.

“Nimeamua kuchukua mwelekeo tofauti wa burudani, ijapokuwa hili halimaanishi kwamba sitakuwa nikitoa nyimbo. Nitaendelea kuwatumbuiza mashabiki wangu kama kawaida yangu, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwa miaka 20 iliyopita,” akasema Kiba.

Baadhi ya watu mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo ni aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, wanamuziki Ommy Dimpoz, Mario kati ya wengine wengi.

Tetesi zinaeleza kuwa kando na Kiba, baadhi ya wasanii katika nchi hiyo pia wanapanga kufungua vituo vya habari.

Miezi kadhaa iliyopita, msanii Harmonize alisema kuwa anapanga kuzindua kituo cha redio.

“Ni kweli. Hata mimi ninapanga kuanzisha kituo changi cha redio,” akasema msanii huyo.

Kiba alijitosa kwenye tasnia ya burudani mnamo 2004, na anafahamika kupitia vibao kama ‘Cinderella’, ‘Usiniseme’, ‘Dushelele’ kati ya vingine vingi.