Makala

Monda roho mkononi Seneti ikianza kumjadili

March 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA CHARLES WASONGA

MASENETA wameanza mchakato wa kuamua hatima ya Naibu Gavana wa Kisii Robert Monda.

Kikao hicho ambacho kimeanza Jumatano kujadili ripoti ya hoja iliyomtimua afisini kimeyumbisha kikao cha pili cha Kamati ya Pamoja ya Haki na Masuala ya Sheria katika Bunge la Kitaifa na Seneti (JLACs) na Kamati ya Seneti Kuhusu Haki, Masuala ya Kisheria na Haki za Binadamu. Kamati hizo mbili zinalenga kuibuka na mfumo bora wa kufanikisha mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco). Kamati hiyo huhitaji angalau wanachama wanane kuendesha shughuli. Watatu hutoka kwa Seneti na watano kwa Bunge la Kitaifa.

Maseneta kwa sasa wanajadili hoja ya kutimuliwa kwa Dkt Monda hivyo hakuna hata mmoja ambaye alifika kwa kamati hiyo. Pia kamati ya pamoja ililenga kuchambua suala tata la kura ya maamuzi na namna ya kuhusisha umma kutoa maoni kwa miswada tisa iliyotokana na ripoti ya Nadco. Kamati hiyo sasa imeratibu Machi 20, 2024, tarehe mpya ya vikao vyake.

Mnamo Jumanne, bunge la Seneti liliamua kuwa maseneta watapiga kura kuidhinisha hoja hiyo au kuitupilia mbali mnamo Alhamisi.

Hii ni baada ya maseneta kupitisha hoja ya kupanga upya shughuli za Seneti ili kutoa nafasi kwa hoja hiyo kushughulikia Jumatano na Alhamisi.

Hoja hiyo iliwasilishwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot ambaye pia ni Seneta wa Kericho.

Kulingana na mabadiliko hayo, Seneti itafanya vikao vya asubuhi na alasiri katika siku hizo mbili–Jumatano na Alhamisi.

“Kikao cha asubuhi kitaanza saa tatu hadi saa saba mchana. Nacho kikao cha alasiri kitaanza saa nane na nusu hadi wakati shughuli zilizoratibiwa zitakamilishwa,” Bw Cheruiyot akasema.

Tayari maseneta wanasikiliza tuhuma dhidi ya Dkt Monda kwa kutoa nafasi kwa bunge la kaunti ya Kisii kuwasilisha ushahidi kuhimili mashtaka yao.

Aidha, maseneta watakuwa na fursa ya kuchanganua mawasilisho kutoka kwa madiwani hao moja kwa moja au kupitia mawakili wao.

Mnamo Alhamisi, itakuwa ni zamu ya upande wa Dkt Monda kujitetea dhidi ya mashtaka hayo kabla ya maseneta kupiga kura kuamua hatima yake.

Mnamo Machi 7, 2024, Seneti iliamua kushughulikia hoja hiyo katika kikao cha bunge lote, baada ya kutupilia mbali hoja ya Bw Cheruiyot iliyopendekeza kubuniwa kwa kamati ya maseneta 11 kuchunguza mashtaka hayo kisha iandae ripoti.

Hii ni baada ya hoja hiyo kukosa kuungwa mkono na seneta yeyote, pale Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna aliyeratibiwa kuiunga mkono kujiondoa.

Kikao cha kuamua hatima ya Dkt Monda kinatarajiwa kushuhudia joto jingi la kisiasa na malumbano makali kati ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio.

Hii ni baada ya Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Silvanus Osoro kutangaza wazi kuwa mrengo wa Kenya Kwanza utafanya juu chini kumsunuru Dkt Monda.

Naibu huyo wa Gavana wa Kisii alichaguliwa pamoja na bosi wake Gavana Simba Arati kwa tiketi ya chama cha ODM, kimojawapo cha vyama tanzu katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni uhusiano kati ya Dkt Monda na Gavana Arati haujakuwa mzuri.

Hii ni baada ya mrengo wa Arati kumsuta naibu huyo wa gavana kwa kushirikiana na Bw Osoro katika kile kilichodaiwa na njama ya kuhujumu uongozi wa Gavana huyo ambaye ni mwandani wa karibu wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Madiwani wa Kaunti ya Kisii walipitisha hoja ya kumtimua Dkt Monda mnamo Februari 29, 2024, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, utoaji hongo na ukiukaji wa Katiba.

Kulingana na sehemu ya 33 ya Sheria za Serikali za Kaunti ya 2013, endapo angalau maseneta 24 wataidhanisha angalau shtaka moja dhidi ya Dkt Monda, ataondoka afisini rasmi.

Na ikiwa mashtaka yote dhidi ya naibu huyo wa gavana hayatapa uungwaji mkono kutoka kwa angalau maseneta 24 wanaowakilisha kaunti, atakuwa amenusurika.

Dkt Monda ni naibu gavana wa pili kutimuliwa afisini na madiwani na hoja yake kuwasilishwa mbele ya Seneti.

Wa kwanza kufikishwa mbele ya Seneti ni Naibu Gavana wa Siaya William Oduol mnamo Desemba 2023.

Hata hivyo, maseneta wa Kenya Kwanza walitumia wingi wao kumnusuru Dkt Oduol ambaye haelewani kisiasa na bosi wake Gavana James Orengo.