Makala

Uvumi kuhusu pilipili ‘nugu’ wapuuziliwa mbali

March 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA MWANGI MUIRURI

MSICHANA mmoja amepuuzilia mbali madai kwamba mmea unazoaa pilipili ‘nugu’ (Kanugu) hupandwa na wachawi au ndege.

Evelyne Wambui wa Gredi ya Sita katika shule ya msingi ya Gakarati iliyoko katika Kaunti ya Murang’a, anasisitiza kwamba yeye mwenyewe ameshaupanda huo mmea hadi ukakomaa kiasi cha kuwa na mavuno.

Bi Wambui anashikilia kwamba dhana nyingi kuhusu pilipili hiyo ni za kupotosha.

Pilipili hii ambayo huwa ndogo saizi ya mbegu ya maharagwe, huwa na ukali wa kipekee.

Kati ya hekaya ambazo husemwa kuhusu pilipili hiyo ni kwamba huwa inapandwa usiku wa manane na wachawi wakiwa uchi.

Wengine hushikilia kwamba mmea huo hupandwa na ndege wale ambao hula matunda kupitia kuangusha mbegu wapitiapo, huku wengine pia wakishikilia kwamba binadamu yeyote akiila anafaa kujisaidia shambani ili mbegu kutoka uchafu wa tumboni mwake zianguke mchangani kisha ziote.

Evelyne Wambui wa Gredi ya Sita katika shule ya msingi ya Gakarati iliyoko katika Kaunti ya Murang’a akionyesha pilipili nugu aliyopanda. PICHA | MWANGI MUIRURI

Lakini msichana Wambui kwa sasa anasema kwamba huo wote ni uongo.

“Mimi nilipotaka kuthibitisha madai hayo, nilichukua pilipili moja mbivu na nikapanda mbegu zake. Ziliota na zikakomaa hadi sasa niko na mavuno ambayo pia nitapanda mbegu zake kuendelea kuthibitisha kwa binadamu wenzangu kuhusu uongo unaosambaziwa wengi,” akasema.

Bi Wambui anasema kwamba imani yake ya Kikristo ndii ilimfanya aulize babake kuhusu imani hizo zinazozingira mmea wa pilipili nugu.

“Babangu aliniambia ni uongo na nilipomwambia anipee ushahidi wake, akanishauri nijaribu kupanda mbegu hiyo,” akasema.

Anashikilia kwamba yeye alipanda mbegu hizo hadharani na anajifamu kwamba yeye sio mchawi wa kuipanda usiku.

“Mimi sikupanda mbegu kupitia njia hizo za kujisaidia shambani na sikupandiwa na ndege. Ni Uongo mtupu,” asema.

[email protected]