Makala

Hatari ya kugeukia waganga kutatua matatizo ya unyumba na ndoa

March 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

NA BENSON MATHEKA

WATU wengi humu nchini wanaendelea kupoteza mamilioni ya pesa wakitafuta suluhisho ya matatizo ya ndoa na unyumba kwa kutafuta huduma za waganga.

Na  ushauri  wanaopata kutoka kwa waganga bandia  umewafanya wengi kujuta baada ya kulaghaiwa pesa na mali yao.

Uchunguzi  wa Taifa Leo umebaini kuwa kuna ‘wataalam’ bandia mitaani wanaodai kwamba wana uwezo wa kutibu maradhi sugu ya upungufu wa nguvu za kiume na kutatua matatizo ya ndoa ikiwa ni kusaidia watu kupata wachumba.

Wataalamu hao wa mitaani wamekuwa wakivuna donge nono hasa kutoka kwa wanaume wanaosumbuliwa na matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume.

Kulingana na utafiti wa shirika  la kimataifa la National Ambulatory Medical Care Survey, NAMCS, umeanika wazi matatizo yanayosababishwa na  upungufu wa nguvu za kiume.

NAMCS  ilifichua kuwa hali hii inachangia ongezeko la talaka na migogoro ya kinyumbani kwa sababu wanaume wengi wamekuwa  hafifu kutekeleza tendo la ndoa.

Kwa mujibu wa utafiti  huo, kwa  kila  wanaume 100,  kuna 75  wanaosumbuliwa na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume hasa wale wenye umri wa kuanzia miaka 40.

Aidha, kutokana na kukithiri kwa tatizo hilo, NAMCS inasema  wanaume wengi wameanza  kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume zinazowadhuru kuongeza matatizo yao ya kiafya.

“Asilimia tano ya wanaume wenye umri wa miaka 40 na zaidi wamekuwa wakihangaika  kutafuta tiba. Na kati ya asilimia 15 na 25 ya wanaume wenye umri wa miaka 65 wanakabiliwa na tatizo hilo,” yaeleza ripoti hiyo.

Nao uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa kuna wanaoamini kuwa kupoteza nguvu za kiume hutokana na uchawi na kugeukia waganga ambao wanatumia fursa hiyo kuwalaghai.

Kulingana na Dkt Ngaruiya Moses, ambaye ni mtaalamu wa afya ya uzazi  katika hospitali ya Scion, Nairobi, hali hii inaweza kusababishwa na kuwepo kwa sehemu  iliyo katika  kiungo cha uzazi cha mwanaume iitwayo corpora cavernosa ambayo kwa sababu tofauti huugua na kumfanya mwanaume kupoteza nguvu.

Anasema kuwa tatizo la upungufu wa nguvu za kufanya mapenzi  huanzia  kwenye ubongo na hata kumfanya mwanaume kupoteza hamu ya kufanya mapenzi na wanaume hawafai kudaganywa na waganga.

Daktari  huyo anaeleza kuwa maradhi ya moyo, figo na kifua yanaweza kumfanya   mwanaume  kushindwa kuwa imara.

Tatizo hili pia huwapata watu walio na shinikizo la damu ambao hukosa nguvu za kiume.

Utafiti wa NAMCS unafafanua kuwa wanaume wanaobugia  pombe kwa wingi , wavutaji wa sigara, watafunaji wa miraa na walipooza mwili  kutokana na maradhi, kunachangia katika hali hii na kuwapelekea waganga pesa na mali waitatue hakuwezi kusaidia.

“Maradhi sugu kama Kisukari, zinaa na kuwa na msongo wa mawazo vinaweza kumfanya mwanamume kushindwa kutekeleza tendo la ndoa na sio uchawi kama waganga wanavyohadaa watu,” asema Dkt Ngaruiya.

Wengine walio katika hatari ya kupata tatizo hili, aeleza, ni wale wenye uzito kupita kiasi huku kati ya asilimia 10 na 20 wakisumbuliwa na tatizo hili kwa sababu ya athari za kisaikolojia.

Kinachotia  wataalamu wasiwasi ni ukweli kwamba wengi wa waathiriwa hawaendi hospitali au kwa wataalamu waliohitmu  kupata ushauri mbali wanawatembelea waganga wanaowahandaa kuwa wana dawa za tatizo hili.

Utafiti wa NAMCS unafichua kuwa wanaume wengi huona haya  kuelezea tatizo hili wasichekwe na kudharauliwa.

“Hata hivyo, ukweli ni kuwa, watu wengi husema uongo ili waonekane kuwa ni wanaume hasa mbele ya wenzao huku wangine wakigubikwa na nadharia duni,” yasema sehemu ya utafiti wa NAMCS.

Daktari Ngaruiya anataja lishe duni  na matumizi ya mihadharati  kama chanzo cha tatizo  hili miongoni mwa vijana.

Nao waganga wamegundua migodi ya pesa kutoka kwa walio na tatizo hili.

Wameweka mabango kujivumisha na hata kulipa matangazo kwenye vyombo vya habari wakijigamba kuwa wana dawa kali za kuongeza nguvu za kiume.

“Hii inadhihirisha hali halisi ilivyo. Ni watu wengi walionaswa na matangazo haya na sasa wanajuta baada ya kutumia pesa nyingi bila kupata afueni,” aeleza  Bw Michael Karanja ambaye ni mwanasaikolojia katika kituo cha Maisha Mema jijini Nairobi.

Wataalamu wanahofia kuwa huenda waganga hawa wakawapatia wateja wao dawa hatari zinazoweza kuwadhuru na hata kuwaua.

“Wako katika biashara na wanaweza kuwapa wanaowatembelea dawa yenye sumu na kuwaangamiza,” asema Bw Karanja.

Na baadhi ya wanaume wanakiri kuwa waliwatembelea waganga hawa kupata tiba ya kupungukiwa na nguvu za kiume.

“Ni waongo. Walinitoza pesa nyingi na sikupata afueni kamwe,” asema mwanaume mmoja aliyeelekezwa na bango moja  kwa ‘daktari’ mmoja mtaani Kinoo.

Mganga huyo aliyedai anatoka Uganda alikamatwa na polisi na kushtakiwa kwa ulaghai na kuhudumu bila kibali.

Mwanamume huyo mwenye umri wa maika 36 asema aliamua kumweleza rafiki yake masaibu yake baada ya mkewe kumtoroka akidai alishindwa kumtimizia tendo la ndoa.

Kulingana na ‘tabibu’ mmoja aliyekubali kuogea na Taifa Leo kwa sharti kuwa tutabana jina lake, wanaume wengi wamekuwa wakifika kwake wakiwa na tatizo hilo.

“Nimewahudumia wengi hapa.  Yangu ni kuwatibu tu na ninaamini wananufaika na huduma zangu kwa sababu idadi ya wateja inazidi kuongezeka,” asema mganga huyo anayeendeshea shughuli zake katika mtaa wa Pipeline, mashariki mwa jiji la Nairobi.

Mganga huyo anaeleza kuwa watu wengi huogopa kwenda hospitali na hilo halimtii tumbojoto.

“Niko hapa niwahudumie. Wengi huja hapa nyakati za usiku na ninawapatia hii dawa,” asema akituonyesha unga aliodai aliutengeneza kutoka kwa mimea ya msituni.

Na Taifa Leo imefichua kuwa wengi wanaotembelea matabibu hawa ni watu walio na uwezo wa kifedha.

“Ninawatoza  kati ya sh 10,000 na 50,000 kwa dawa ya mwezi mmoja,”asema.
Kupungua kwa nguvu miongoni mwa wanaume wengi kumesababisha wengi wao waishi katika maisha na hali ya kusononeka na wengine wameripotiwa kujiua kutokana na hali hiyo.

Wataalamu wa afya na wanasaikolojia wanaamini kuwa mara nyingi hali  hiyo, hasa kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 45, husababishwa na msongo  katika akili hasa  wasiofanya kazi  nyingi.

“Watu wengi wanaofikiri kuwa wamepungukiwa na nguvu hizo huwa wako sawa,” yasema sehemu moja ya utafiti uliofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Havard, nchini Amerika.

Utafiti huo unafafanua kuwa tatizo la watu hao huwa ni kushiriki tendo hilo kwa wakati usiofaa.

“Wanashiriki wakiwa hawajajitayarisha kiakili,” wasema utafiti wa wataalamu wa Harvard.

Wataalamu hao wanaeleza kuwa tatizo hilo huwapata wanaume wengi kwa sababu ya utumiaji wa vyakula vyenye kuongeza kiwango kikubwa cha mafuta mwilini ambao hawashiriki katika mazoezi ya viungo ambayo huifanya misuli ya damu mwilini kutokufanya kazi vizuri na hivyo kusababisha matatizo mengi ya mwili kushindwa kufanya kazi zake ipasavyo.

Na kuna hofu kuwa idadi ya wanawake wanaowatembelea waganga kusuluhisha matatizo ya ndoa imeongezeka. Katika kisa kimoja, wanawake wawili walilaghaiwa zaidi ya Sh30,000 na wanaume waliodai kwamba wangetatua shida zao za ndoa eneo la Meru.

Sawa na kisa cha Kinoo waganga hao walikamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa kosa hilo. Kwa mujibu wa Bw Karanja waganga wanaolenga walio na matatizo ya ndoa wamekuwa wakifanya biashara nono.

“Wamekuwa wakivumisha huduma zao kwa sababu wanajua kuna wateja hapa nchini. Kuna haja ya kampeni kufanywa ili kuwaeleza watu ukweli wa mambo na wanayopasa kufanya wakipatwa na matatizo kama haya,” akasema.

Anasema inasikitisha kuona raia wa kigeni wanaweza kuja nchini kulaghai watu kwa kujifanya waganga walio na uwezo wa kutatua shida zao za unyumba na ndoa.

“Katika karne hii, jambo kama hilo halifai kutendeka nchini,” akasema.