Bambika

‘Ladha ya ndoa ya wake wengi ni kuwa wa kwanza’

March 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMKE mmoja ambaye aliolewa mke wa tatu, amedai kwamba ladha ya ndoa ya aina hiyo ni “wewe mwanamke kuwa wa kwanza”.

Bi Nyambura Wahu ana tajriba katika ndoa iliyo na zaidi ya mke mmoja, yeye akiwa ni wa tatu kwa mumewe Bw Ngonya wa Gakonya ambaye kwa sasa ni marehemu.

Bi Wahu anasema raha zaidi kwake ingejitokeza ikiwa angechukua nafasi ya kwanza.

Aliolewa akiwa na umri wa miaka 21 na mume wake kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka 52.

Licha ya kujipata kwenye ndoa ya mitara, ombi lake na ushauri kwa wanawe wa kike ni kuwa wasiwe wake wa pili au wa tatu.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 57 anasema kuwa alifanikiwa kupata watoto 10.

Mumewe aliaga dunia na kumuachia watoto wadogo wanne.

Nchini Kenya wanawake wengi wanajulikana kupinga ndoa za mitara, japo kuna wengi ambao wako tayari kuwa mke wa pili, wa tatu au wa nne. Wengine wanacheza chini ya maji, wakihiari kuwa mipango ya kando.

Wake hao wakipata pingamizi na kukejeliwa kwa kuwa kizingiti cha maendeleo kwenye familia.

Bi Nyambura Wahu kwenye mahojiano na Taifa Leo. PICHA | FRIDAH OKACHI

Mke wa tatu alitambuliwa kama akiiera ama mka, nyumba ambayo ilimpa amani mwanamume kutokana na matatizo yanayompata.

Bi Wahu aliambia Taifa Leo akiwa Dagoretti kwamba sababu ya ndoa hizo kutokea, ni kutokana na changamoto kama vile mwanamume kukosa kupokelewa vizuri na mkewe, au pesa na mali chungu nzima ikisukuma wanaume kutafuta mke mwingine.

Anasema kuolewa kuwa mke wa tatu kulimpa stahamala kwani alipitia nyakati ngumu na mambo mazito.

Anawashauri wanawe wa kike na mwanamke mwingine kivyovyote vile kutafuta ile ya kwanza na wakiweza, wamtunze mume asione haja ya kumuoa mke mwingine.

“Kila wakati mimi huambia mabinti zangu kung’ang’ania nafasi ya kwanza… ya pili na tatu utaonyeshwa moto sana,” akasema Bi Wahu.

Bi Wahu anaeleza jamii ya Agikuyu ilimruhusu mwanamume kuwa na wake zaidi ya watano.

Anasema nafasi ya kwanza inamuepushia mwanamke vita vingi.

“Ukiwa wewe ndiye mdogo, unaweza ukajiona mume anakupenda kuliko wenzako lakini baadaye mambo yanaweza kubadilika,” akasema.

“Kitambo mume alikuwa akioa hata wanawake saba na wakati wa kurejea nyumbani akitoka kazini au shughuli nyingine, hao wake wote walikuwa wakimkimbilia na kumwamkua. Kisha kila mmoja anarudi kwake akiwa na furaha,” akaeleza.