Makala

Sababu za manahodha kupenda jeti mbovu wakihepa bandari za kisasa

March 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUME KAZUNGU

JETI nyingi ndogo na kuukuu kisiwani Lamu zimeibukia kupendwa kutumiwa na manahodha wengi wa mashua na maboti katika harakati zao za kila siku za kupandisha au kushukisha abiria na mizigo.

Lamu ina zaidi ya jeti 10 zipatikanazo kwenye maeneo tofauti tofauti.

Miongoni mwa jeti hizo ni zile kubwa na za kisasa zilizokarabatiwa na serikali kuu.

Jeti hizo ni Mokowe iliyojengwa kwa kima cha Sh599 milioni, Manda iliyogharimu Sh48 milioni, Mtangawanda iliyojengwa kwa Sh72 milioni, ile ya KPA kisiwani Lamu iliyojengwa kwa karibu Sh300 milioni na Mangrove Jeti iliyokarabatiwa kwa kima cha Sh35 milioni.

Aidha jeti ndogo za Lamu ambazo manahodha wamekuwa wakizikimbilia kuzitumia kila siku ni ile ya mbele ya Mkahawa wa Bush Gardens Seafront Hotel and Restaurant, zile zilizoko mbele ya hoteli za Lamu Palace na Labanda, Jeti ya mbele ya afisi ya Captain Andys, ile ya mbele ya mkahawa wa Tamarind na pia jeti ya afisi za zamani za KenGen.

Jeti nyingine ndogo na zilizozeeka japo zimeibukia kupendwa Lamu ni ile ya kando kando ya jeti mpya ya Mokowe, Jeti ya Ng’ombe pia ikiwa Mokowe, jeti ya Kizuke miongoni mwa nyingine nyingi.

Kila unapopita kwenye jeti hizo, utapata manahodha na utingo wakijituma kupakia na kupakua mizigo, kushukisha au kupakia abiria nakadhalika.

Yaani jeti hizi kuukuu ndizo ambazo ziko bizi zaidi ikilinanishwa na zile bandari mpya na za kisasa.

Lakini je, ni nini sababu zinazowasukuma manahodha Lamu kupenda kutumia sana jeti mbovu na kukwepa bandari za kisasa?

Ali Shekue,nahodha, alisema mapenzi yao kwa jeti mbovu au kuukuu yanatokana na kwamba mara nyingi jeti husika zinakosa msongamano wa watumiaji ikilinganishwa na zile bandari mpya zilizoko Lamu.

Bw Shekue alisema badala ya kupoteza muda mwingi kupanga foleni kwenye bandari au jeti kubwa za kisasa kutokana na idadi kubwa ya wanaozitumia, wao uisia kwenda kutumia jeti ndoo na mbovu ambazo hazina misongamano yoyote.

“Twapenda hizi jeti ndogo zinazoonekana kuwa mbovu na zilizotelekezwa.  Hapa mara nyingi huwa hakuna misongamano ya abiria na mizigo. Waweza kushukisha abiria au mizigo ukitumia muda mfupi ikilinganiswa na bandari kubwa kubwa ambapo twalazimika kukaa dakika kadhaa tukingojana kushukisha na kupakia abiria na mizigo kwa zamu,” akasema Bw Shekue.

Sababu nyingine inayowasukuma manahodha kukimbilia kutumia jeti mbovu na ndogo ni kwamba licha ya jeti hizo kujengwa zamani, muundo wake ni dhabiti zaidi ikilinganishwa na jeti au bandari kubwa za kisasa.

Kulingana na Bw Omar Musa, ambaye ni nahodha pia, jeti zilizojengwa hivi majuzi zimekuwa na changamoto ya kubomoka au kupasuka kiholela, hivyo kuwafanya watumiaji kuziogopa.

“Ukiangalia muundo wa zamani ulioundiwa hizi jeti ndogo ni dhabiti. Haziharibiki au kupasuka vivi hivi licha ya kuwa za jadi. Ukitazama jeti kama vile ile ya KPA tayari boya lake limekatika, hivyo ni vigumu kwetu kuitumia jinsi ilivyo. Na ndiyo sababu tunakimbnilia hizi jeti ndogo na za zamani,” akasema Bw Musa.

Manahodha pia wanataja mazoea kuwa miongoni mwa sababu zinazowasukuma kutumia jeti mbovu na za zamani.

“Tumezoea tu hizi jeti za zamani. Ni rahisi kwetu sisi manahodha kutia nanga vyombo vyetu hapa kinyume na zile bandari kubwa na za kisasa,” akasema Bw Kassim Twalib, nahodha.

Kaunti ya Lamu in zaidi ya manahodha 6,000 wa maboti na mashua.