AUC: Mbele iko sawa kwa Raila
NA AGGREY MUTAMBO
AZMA ya kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kuwania wadhifa wa Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Afrika (AUC) imepata nguvu baada ya kikao cha Addis Ababa kuondoa kikwazo cha suala la jinsia kwa wagombea.
Kwenye kikao hicho maalum kilichoandaliwa Ijumaa, uamuzi uliafikiwa ambao sasa utafanya Bw Odinga kushusha pumzi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi, hitaji kwamba mwenyekiti ajaye wa AU awe mwanamke limeondolewa.
Vilevile ilikubaliwa katika kikao hicho kwamba mwenyekiti mpya awe ni wa kutoka Afrika Mashariki. Ingawa hivyo, kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) itaamua yenyewe wagombea wa kujitosa uwanjani.
“Hizi ni habari nzuri kwa eneo la Afrika Mashariki kutoa wagombea wa kiti cha Mwenyekiti wa AUC,” alisema Bw Mudavadi katika taarifa.
Uamuzi wa Baraza la AU sasa ni sharti uidhinishwe na marais na viongozi wa nchi wanachama wa AU.
AU ina wanachama 55.
Tangu 2021, AU ilikuwa imeafikia makubaliano kwamba Naibu na Mwenyekiti wa AUC wawe wa jinsia tofauti.
Lakini hayakuwepo makubaliano yoyote kwamba jinsia liwe ni suala la kupokezana kutoka kwa Mwenyekiti mmoja hadi mwingine. Kwamba akitoka mwanamume aingie mwanamke.
Mwaka 2018, makubaliano yaliafikiwa kwamba maeneo yawe yakipokezana fursa ya kutoa Mwenyekiti ambapo maeneo yaliorodheshwa kama kanda ya Afrika ya Kati, kanda ya Mashariki, kanda ya Kaskazini, kanda ya Magharibi na kanda ya Kusini.
Mwenyekiti wa sasa wa AUC Moussa Faki Mahamat anatoka Chad katika kanda ya Afrika ya Kati na naibu wake ni Monique Nsanzabaganwa wa Rwanda katika kanda ya Afrika Mashariki.
Kanda ya Kaskazini ndio pekee itakayotoa wagombea wa kiti cha unaibu.