Makala

Matapeli wanavyotumia watoto na walemavu kuvuna pesa

March 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 4

NA BENSON MATHEKA

MIJI mikubwa nchini imegeuka kuwa makao ya watu wanaotumia hila na ujanja kupata pesa kwa kuombaomba wakijifanya wana shida au ulemavu.

Imebainika kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaochuma  maelfu  ya pesa kutoka  kwa wakazi wa jiji kwa kutumia mbinu mbalimbali.

Na wakazi wameelezea kutofurahishwa na watu hao hasa baada ya kufichuliwa kuwa baadhi yao hutumia watoto walemavu kupata maelfu ya pesa kila siku.

Wakazi wa jiji la Nairobi wanasema kuwa  idadi ya watu wanaotumia ujanja kupata pesa imeongezeka mno katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kinachowakasirisha wakazi hao ni kugundua kuwa hata watu kutoka nje ya nchi wamekuwa wakimiminika nchini kuombaomba mitaani.

“Nilishtushwa na habari kwamba watu kutoka Tanzania wanakuja kuombaomba nchini. Huku ni kutumia ukarimu wa Wakenya vibaya,” asema Calvin Missingo, mkazi wa mtaa wa Komarock jijini Nairobi.

Missingo asema kuwa kilichomuudhi zaidi ni kutambua kuwa watu wazima wanatumia watoto walemavu ambao ni maskini kujipatia pesa.

Missingo anayehudumu na shirika moja la kijamii anasema kuwa watu hao wanakosa utu kwa kuwanyima watoto walemavu mahitaji ya kimsingi huku wakijipatia pesa kwa njia za mkato.

“Ni laana kubwa kuwatendea watoto unyama huo,” asema Missingo.

Ingawa sio wote wanaotumia hila kuombaomba mitaani, imefichulika kuwa baadhi ya watu hujifanya kuwa walemavu au wamelemewa na matatizo kujipatia pesa za kutumia katika starehe zao. Na hata walemavu halisi waombao katika barabara za jiji hawafaidiki na pesa wanazokusanya.

Wengi wao hutumiwa na watu kuwakusanyia pesa.

Mwanaume mmoja tuliyempata karibu na kituo cha mabasi cha Ambassador alisema kuwa huwa anampelekea ndugu yake pesa anazokusanya.

“Ndugu yangu huchukua pesa zote ninazopewa na watu. Huwa ananinunulia chakula tu,” aliambia Taifa Dijitali na kuongeza kuwa ndugu yake, aliyekataa kumtaja jina hafanyi kazi.

“Huwa ananileta jijini alfajiri na kunichukua jioni. Tunategemea pesa ninazotupiwa na wasamaria wema kwa mahitaji yetu,” akadokeza jamaa huyo tulieyabana majina yake kwa sababu za kiusalama.

Mwanaume huyo alisema hupata kati ya Sh1, 000 na Sh3, 000 kwa siku moja.

Katika uchunguzi wetu, tulimfuata jamaa mwingine tuliyempata akiomba katikati mwa jiji hadi eneo la Congo mtaani Kawangware, tulipompata jioni akipiga mtindi katika kilabu kimoja cha kuuza busaa.

Wanaomjua jamaa huyo walishangaa tulipowaambia kuwa huwa anaombaomba jijini.

“Hapana. Huyu jamaa hutuambia kuwa yeye ni dereva katika kampuni moja eneo la viwandani,” alisema mwanaume mmoja aliyesema ni rafiki wake wa karibu.

Cha ajabu ni kwamba jamaa huyo huwa na mabango yanayoelezea jinsi alivyoshindwa kupata pesa za kulipia matibabu nchini ng’ambo, jambo linalogusa watu wengi na kumchangia.

Mbali na wanaojifanya kuwa wagonjwa na walemavu, kuna kundi lingine la watu wanaovalia nadhifu wanaozunguka barabara za jiji wakisingizia kuwa wamekosa nauli ya kuwafikisha wanakoenda.

Watu hao huwasimamisha watu na kuwaomba wawasaidie kwa pesa huku wakiongea kwa upole wahurumiwe. Ajabu ni kwamba wanaweza kuomba mtu mmoja hata mara kumi!

“Wamekuwa kero kwa wakazi wa jiji. Wanakusanya pesa nyingi kutoka kwa watu wanaowaonea huruma,” asema Juma Ndeta, anayedokeza kuna jamaa aliyezoea kumuomba pesa katika barabara ya Harambee Avenue jijini Nairobi kila siku kwa kudai kuwa ameporwa.

“Nilipogundua kuwa alikuwa tapeli, nilimkaripia. Kutoka siku hiyo, sijamwona tena. Pengine alihamia kwingine,” asema Ndeta aliye afisa wa uhusiano mwema katika kampuni moja jijini.

Ndeta asema kuwa mbinu za kujipatia pesa kwa njia za mkato zinakua kwa kasi na huenda zikabadilika na kuwasababishia wakazi wa jiji hatari kubwa.

“Ni rahisi kwa watu kama hao kujiingiza katika uhalifu na kuwahangaisha watu,” asema.

Tumebaini kuwa ombaomba jijini wamegawanyika katika jinsia na rika tofauti. Cha ajabu ni kwamba wengi  wao  ni watu wazima wanaoweza kufanya aina tofauti za kazi.

Kulingana na Ndeta, Serikali inapaswa kuwachukulia hatua za kisheria wanawake wanaowatumia watoto wao kuomba pesa katika barabara za jiji.

Wanawake hao hulenga maeneo yaliyo na maduka makubwa na kuwatuma watoto wao kuomba pesa kwa wateja wanaotembelea maduka hayo.

Wengine huwaweka watoto wa umri mdogo katika hatari kubwa kwa kuwaambia waombe madereva wakati magari yamesongamana barabarani.

Katika tukio moja karibu na duka la Naivas kwenye makutano ya barabara za Kenyatta na Moi, tulishuhudia mwanamke mmoja akimchuna msichana wa miaka mitano kwa kushindwa kupata pesa kutoka kwa wapita njia.

“Leo hutakula wewe,” alimfokea msichana huyo aliyekuwa akilia.

“Watoto hawa wanapaswa kuwa shuleni lakini wazazi wao wanawatumia kupata pesa. Ni jambo ambalo Serikali inapaswa kuchunguza na kuwachukukulia hatua wanaohusika,” asema Ndeta.

Kwa baadhi ya watu jijini,  hiyo imekuwa  ajira rasmi.

Hawaoni aibu wakitumia ujanja na hata nguvu kujipatia pesa kwa kuvuna wasikopanda.

Awali ni wanaume pekee waliojulikana kwa kutumia mbinu tofauti za kujipatia pesa kwa njia za mkato lakini sasa, mambo yamebadilika. Wanawake na hasa wasichana wamekuwa katika mstari wa mbele kutumia njia za hadaa kupata pesa.

“Wamegundua kuwa wanaume wanaguswa msichana akiomba msaada. Wanaume wengi wamekuwa wakiangukia mitego yao. Wasichana wanaoshiriki biashara hii wameongezeka siku hizi,” asema Peter Onyango anayedai kuwa alipoteza Sh10,000 kwa kuangukia mtego wa mwanamke.

“Aliingia katika kilabu nilichokuwa nikiburudika kwa vinywaji katika barabara ya Luthuli. Aliniambia kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza jijini na alikuwa amepoteza kila kitu.

“Kwa kumhurumia, nilijitolea kumuonyesha kituo cha magari ya kwenda mtaa wa  Huruma alikosema alinuia kuishi na rafiki yake. Hatua chache kabla ya kufika kituoni, nilivamiwa na wanaume wawili. Walinishika kwa nguvu huku mwanadada huyo akinipora” aeleza Onyango.

Kinachochochea watu kushiriki tabia hii ni umasikini, ukosefu wa ajira na uzembe uliopo miongoni mwa wakazi wengi wa sehemu za mijini.

“Watu wengi wanabuni njia za rahisi za kujipatia pesa wanapokosa kazi. Wengine ni wazembe kupindukia isipokuwa midomo yao iliyo miepesi kulaghai. Vile vile, umasikini uliokita mizizi katika idadi kubwa ya wakazi wa mijini umepelekea wengi kuamua liwe liwalo na kuhadaa wapate hela,” asema Bi Joyce Muthoka, mkurugezi wa shirika moja la kijamii jijini.

Muthoka asema kuwa kuna kazi nyingi baadhi ya walemavu wanaweza kufanya wakipatiwa mafunzo na mtaji wa pesa unaohitajika.

“Tunachohitaji ni sera madhubuti ya kuwapatia mafunzo na pesa na wengi wao watajitegemea,” asema na kuongeza kuwa ni heri kumfunza mtu mbinu za kuvua samaki kuliko kumpatia kipande cha samaki.

“Ninajua walemavu wengi waliodhaniwa hawawezi kujimudu ambao baada ya kupokea mafunzo wanajitegemea,” anasema.