Habari za Kitaifa

Wakenya kuanza kuvuna pesa kupitia Facebook na Instagram

March 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto mnamo Jumatatu Machi 18, 2024 alisema kuwa wasanii na Wakenya wanaotumia mitandao ya Facebook na Instagram kuendeleza sanaa zao, wataanza kupata pesa kutokana na matumizi yake kuanzia Juni mwaka huu.

Malipo hayo yatakuwa yakitolewa na kampuni ya Meta, inayomiliki mitandao hiyo miwili.

Rais Ruto alisema kuwa malipo hayo yatakuwa yakitumwa kwa njia ya M-Pesa.

Akizungumza Jumatatu, Rais Ruto alisema kuwa kampuni hiyo imefanya majaribio kuhusu mfumo huo, ambapo tayari umefaulu.

Alisema baada ya kampuni hiyo kuweka vigezo vya wale watakaotimiza masharti ya kulipwa kukamilika, wasanii hao wataanza kupokea malipo yao kwa njia ya M-Pesa.

Alisema moja ya changamoto kubwa ambayo wasanii wa mitandaoni nchini wamekuwa wakipata ni ukosefu wa mfumo thabiti kupokea malipo yao.

“Nina furaha kubwa kwamba malipo hayo yataunganishwa na kutumwa kwa mfumo wa M-Pesa. Ninafikiri watu wengi wanashangaa kuhusu vile tutafanikiwa kutekeleza haya ilhali wasanii wetu wengi wana kadi za malipo au njia nyingine za malipo. Hata hivyo, nilifurahi sana wakati kundi kutoka Meta liliniambia limefanya majaribio kupitia mfumo wa M-Pesa na ukafaulu,” akasema Rais Ruto.

Alisema hayo alipokutana na maafisa kutoka kampuni ya Meta, inayomiliki mitandao ya Facebook na Instagram. Kampuni hiyo ina makao yake nchini Amerika.

Wasanii kadhaa pia walikuwa kwenye kikao hicho.

Wakati wa mazungumzo hayo, maafisa hao walisema kuwa kufikia Juni 2024, wasanii wa mitandao kutoka Kenya wataanza kupata malipo yao kwa kazi ama video wanazoweka katika mitandao hiyo.

Rais Ruto amekuwa akijaribu kushinikiza vijana kutumia mitandao kama njia ya kupata ajira.