Habari za Kitaifa

‘Wana’ wa Ruto wakabana koo kuhusu madai ya hongo ya Sh13 bilioni

March 18th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

WAZIRI wa Uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen na Seneta wa Nandi, Samson Cherargei wameendeleza uhasama wao, wawili hao ambao ni wandani wa Rais William Ruto wakishambuliana hadharani.

Wamekabana koo, Bw Murkomen akilalamikia Seneta Cherargei kwa kumharibia jina kwa madai kuwa waziri huyo aliumishwa hongo ya Dola 100 milioni za Amerika (sawa na Sh13.425 bilioni thamani ya Kenya) na mwanakandarasi raia wa Uchina alipokuwa ziarani nchini humo 2023.

Hata baada ya Bw Mukormen kumsihi Cherargei amuombe msamaha na kufutilia mbali madai hayo katika mitandao ya kijamii, Waziri ameeleza katika kesi aliyomshtaki katika Mahakama ya Milimani kwamba Seneta huyo alikataa na “badala yake kumtaka wakutane kortini mbivu na mbichi zijulikane.”

Sasa kesi imewasilishwa mahakamani na jukumu la Bw Cherargei sasa likiwa ni kuwasilisha ushahidi kuthibitisha madai kuwa Murkomen alipokea hongo.

Katika kesi aliyoshtaki, amesema kwamba matamshi ya Bw Cherargei ni ya uwongo na yanalenga kumharibia sifa na jina tu.

“Matamshi ya Cherargei ni ya uwongo na yana mtazamo wa kunichafulia jina kama Waziri katika Serikali ya Kenya Kwanza, Wakili mwenye tajriba ya juu na mtu wa familia,” asema Bw Murkomen katika kesi aliyowasilisha katika Mahakama ya Milimani.

Waziri huyo amedokeza kwamba matamshi hayo ya uwongo aliyotamka seneta huyo mwaka uliopita

yalimkejeli, kumharibia sifa na jina ikitiliwa maanani yeye ni mtu mwadilifu na mwenye familia.

Waziri Murkomen alisema Bw Cherargei amedumisha kwamba madai hayo kuhusu hongo anayosemekana kupokea ni ya kweli.

Waziri alidokeza kuwa Cherargei alisema alikuwa tayari wamenyane kisheria.

“Madai hayo yameshusha hadhi yangu na ninamtaka Cherargei ayathibitishe,” alisema Bw Murkomen.

Aidha, Murkomen amewasilisha ushahidi kwamba mnamo Novemba 24, 2023, Cherargei aliitisha mkutano na wanahabari na kutoa matamshi hayo ya uongo kwamba “nilipokea hongo kutoka kwa wanakandarasi wa Uchina nilipokuwa ziarani mle.”.

Bw Cherargei alimtaka Bw Murkomen akane ama kukiri madai hayo kwamba alitia kibidoni Dola 100 milioni kama hongo kutoka kwa mwanakandarasi wa Kichina.

Bw Murkomen anaomba mahakama imwamuru Cherargei amlipe fidia na kumuomba msamaha kupitia vyombo vya habari.