Michezo

Mashabiki wa Shabana FC wamlilia Mungu asaidie isishushwe ngazi

March 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WYCLIFFE NYABERI

MASHABIKI wa Shabana FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Nchini (FKF-PL) sasa wamemgeukia Mungu kumwomba asaidie klabu hiyo kukwepa shoka la kushushwa ngazi kurudi kwa Ligi ya Supa (NSL).

Zaidi ya mashabiki 100 wa Shabana wikendi iliyopita walizuru eneo la Ngong Hills kuwatilia dua wachezaji wa timu hiyo kama njia moja ya kujaribu kusitisha msururu wa matokeo mabaya ambayo timu hiyo imekuwa ikiandikisha.

Shabana ilileta msisimko pale iliposhinda taji la NSL mwaka 2023 na kupandishwa ngazi kushiriki katika ligi kuu ya Kenya.

Lakini timu hiyo yenye ufuasi mkubwa Kisii haijaonyesha fomu iliyokuwa nayo katika NSL na sasa inashikilia nafasi ya 17 katika jedwali la timu 18 ikiwa na pointi 18 pekee.

Wakiwa wamechoka kuona timu yao ikikaa katika nafasi hiyo ambayo ni ya kushushwa ngazi, mashabiki walizuru eneo hilo kumuomba Mungu asaidie timu hiyo isalie kwenye ligi kuu msimu ujao.

“Mwenyezi Mungu, tunakuomba usaidie timu yetu ya Shabana isishushwe ngazi na ianze kuandikisha matokeo ya kuridhisha. Hatutaki tena irudi nyasini,” shabiki mmoja alisikika akiomba.

Walipiga sala hizo katika makundi makundi, huku wakiwa wamevalia jezi za timu hiyo.

Mashabiki wengine wanapanga kufanya maombi mengine Jumapili katika vilima vya Manga vilivyoko katika Kaunti ya Nyamira.

Vilima hivyo vina historia kubwa kwa watu wa jamii ya Abagusii kwani zama za kale, wenyeji walikuwa wanavizuru na kufanyia maombi hapo, wakiomba shida zilizokuwa zikiwakumba ziwaondokee.

Baada ya kugaragaza mechi 24, ‘Tore Bobe’ kama Shabana wanavyofahamika, wamefanikiwa kuonja ushindi mara nne tu. Wamepiga sare sita na kulimwa katika mechi nyingine 14.

Ligi Kuu imebakisha mechi 10 kutamatika na kufikia sasa, juu jedwalini kuna miamba wa soka nchini Gor Mahia ambao wamejinyakulia alama 50 baada ya kujimwaya uwanjani kwa mechi sawa na za Shabana.

Wasimamizi wa Shabana hawaelewi ni kwa nini haiandikishi matokeo ya kuridhisha licha ya kuweka mikakati yote faafu kwa wachezaji na benchi ya kiufundi.

Mkufunzi wa Shabana Sammy Omollo ‘Pamzo’, alipopewa mikoba ya kuidhibiti mapema mwaka 2024, aliwahakikishia mashabiki kuwa alikuwa na uwezo wa kuikwamua kutoka eneo hilo hatari lakini bado wananing’inia huko.

Nzoia United wanavuta mkia jedwalini kwa alama 17.