Habari za Kaunti

Monda aelekea kortini kupinga kubanduliwa kwake

March 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WYCLIFFE NYABERI

ALIYEKUWA Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Dkt Robert Monda ameelekea kortini kupinga kung’atuliwa kwake afisini.

Hata hivyo, Jaji Teresia Achieng Odera wa Mahakama ya Kisii, ambapo kesi hiyo iliwasilishwa, hakutoa maagizo yoyote.

Badala yake, Jaji alimweleza Mbunge huyo wa zamani wa Nyaribari Chache kuwasilisha kujulisha Seneti na wahusika wengine katika kesi hiyo na kisha arejee kortini mnamo Machi 26, 2024, ili kesi yake isikiLIzwe.

“Nimezingatia kwa makini ombi la Machi 18, 2024. Kusikiza kwa kesi kati ya pande zote kutafanyika Machi 26, 2024,” Jaji Odera alisema.

Bunge la Seneti wiki jana Alhamisi usiku liliidhinisha mashtaka yote manne dhidi ya Dkt Monda jinsi yalivyoletwa na Bunge la Kaunti ya Kisii.

Hii ilimfanya kuwa naibu gavana wa kwanza kuondolewa afisini tangu kuanzishwa kwa vitengo vya ugatuzi mwaka 2013.

Kiini cha tuhuma zilizosababisha Dkt Monda kufungishwa virago ni rushwa ya Sh800,000 kutoka kwa Denis Mokaya kwa ahadi kwamba angempatia kazi ya Umeneja wa Mauzo katika Kampuni ya Maji na Maji-taka ya Gusii (Gwasco) pamoja na kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa kaka yake, Reuben Monda, kwa kukata miti katika ardhi ya familia yao.

Maseneta hao walipiga kura kwa wingi kuunga mkono mashtaka yote manne yaliyotolewa dhidi yake. Ni pamoja na ukiukaji mkubwa wa Katiba, matumizi mabaya ya afisi, utovu wa nidhamu uliokithiri na uhalifu chini ya sheria za kitaifa.

Kufuatia kutimuliwa kwake, sheria ilimpa gavana Arati siku 14 za kuteua naibu mpya ikiwa uamuzi huo haungepingwa mahakamani.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake katika Seneti, wabunge hao walichana utetezi wa Dkt Monda kwa kutilia shaka uhalali wake wa kushikilia wadhifa wa umma.

Maseneta Enoch Wambua (Kitui), Joe Nyutu (Murang’a) , Wahome Wamatinga (Nyeri), Okong’o Omogeni (Nyamira), Boni Khalwale (Kakamega), Tabitha Karanja (Nakuru) na Hamida Kibwana (maalum) walipigia debe hoja Dkt Monda afurushwe.

[email protected]