Maoni mseto kuhusu mbinu ya ukandaji kutumia taulo ya moto
NA FRIDAH OKACHI
TIBA ya kukanda mwili imekuwepo kwa muda mrefu sana, asili yake ikihusishwa na mataifa kama vile India, China, Japan na Misri.
Nchini Kenya, tiba hii inazidi kukua na kubadilika kadri muda unavyosonga.
Sasa kuna aina mpya ya ukandaji ambapo mteja hulala kisha mtaalamu anapitisha taulo ya moto juu kwenye ngozi.
Ukandaji huo unaotumia taulo ya moto unavutia wateja kutoka kaunti mbalimbali ambao wanafunga safari hadi Kaunti ya Mombasa kupata huduma hizo.
Bw Benson Muriithi,33, anayetoa huduma hizo jijini Mombasa, aliambia Taifa Leo aina hiyo ya ukandaji imekubaliwa na wengi.
Faida zake kwa mteja ni nyingi, ikiwa ni pamoja na kuondoa makunyanzi, kumaliza maumivu ya viungo, kupunguza hali ya mtu kuhisi usingizi kila mara, kusaidia usagaji wa chakula tumboni, na kupunguza unene. Pia hutumika kama tibu ya mafua.
“Ukandaji huu unafahamika kitaalamu kama ‘fiery towel massage’ na ni mbinu maalum ya kuponya maumivu mbalimbali kwenye mwili wa mteja,” akaeleza Bw Muriithi.
Aidha, alisema kuwa wapo baadhi ya wateja wake wanaoingiwa na hofu kuona moto. Huwa ana kibarua kizito kuwashawishi kwamba hakuna cha kuhofu.
“Nilipoanza kutoa huduma hii, wateja wengi waliogopa aina hii ya ukandaji mwili inaweza kuleta madhara, lakini ukweli ni kwamba haina madhara kwa mwili,” akasema.
Alisema mteja asiye na ujasiri akisikia taulo inawekwa mafuta fulani ya kuwaka moto, anaondoka ghafla.
Lakini alisema hali inaanza kubadilika na wateja wanakumbatia ‘teknolojia’ hiyo ya ukandaji.
“Ni moto lakini hauwezi kukuchoma ikizingatiwa kwamba ni shughuli inayofanywa na mtaalamu. Mara tu huduma hii inapokamilika, mteja anahisi akiwa na utulivu zaidi,” akasema.
Lakini alisema mara nyingi huduma zake hulenga watu walio na matatizo ya mgongo na magoti.
Mteja wake mmoja, Bw Nick Kamau ambaye alisafiri kutoka jijini Nairobi hadi Mombasa kusudi apate huduma hizo, alisema maumivu ya mgongo ndio yalimpelekea kutafuta huduma hiyo.
“Mwanzoni niliogopa lakini nilipowekewa kitambaa cha kwanza, cha pili na moto kuwaka, kisha akaongezea cha tatu, nilihisi kuwa na utulivu,” alisema Bw Kamau.
Nje ya kituo hicho, kwenye barabara ya Moi Avenue, Bi Lydia Virginia, alikuwa hapo nje lakini akaambia Taifa Leo kwamba hawezi kutafuta huduma hizo.
Alisema anaogopa huenda huduma hizo zikakatiza maisha yake upesi.
“Sisi wa kizazi cha leo tumekuwa wa kukimbilia kila kitu tunachoona. Binafsi acha nibaki na maumivu yangu kwa sababu huo moto ukiwaka juu ya ngozi yangu, mambo yangu yatakuwa yameisha,” Bi Virginia akasema huku akicheka.
Lakini mmiliki wa biashara yenyewe alisema siku za wikendi, hupokea zaidi ya wateja 20 wanaotafuta huduma hiyo ya ukandaji.
Wataalamu wanapendekeza kufanyiwa ukandaji wa mwili angalau mara moja kila baada ya wiki tatu ili kusaidia kuboresha afya na kupunguza maumivu yanayoweza kutokana na mazoezi makali ambayo mwili huwa umepitia.