Makala

Mama anayejituma kufufua kilimo cha mimea asilia

March 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SAMMY WAWERU

JEPHLINE Ojwang’ ni mkulima wa mimea asilia katika Kaunti ya Migori, shughuli za zaraa anazojivunia kukumbatia. 

Anaendeleza kilimo kupitia kundi la kina mama, Rongo Livelihood Women’s Group, ambapo hukuza njugu karanga, mihogo, na mseto wa mboga za kienyeji kama vile mchicha (terere) na kunde.

Kando na kundi hilo lenye wanachama 22 kuwawezesha kujipa mapato, Jephline anasema lengo la uasisi wake pia lilikuwa kuhamasisha urejeleo wa vyakula vya kienyeji.

“Tulianza tukiwa wanachama 30, japo kwa sasa tumesalia 22 na tunajivunia uzalishaji wa chakula cha jadi,” anasema.


Jephline Ojwang’ akionyesha mbegu za mihogo. PICHA|SAMMY WAWERU

Rongo Livelihood Women’s Group inahudumu kupitia Shirika la Kijamii la Community Mobilization Against Desertification (CMAD), shabaha yake ikiwa kukabiliana na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi (climate change) katika sekta ya kilimo.

Jephline anakuza mseto wa mimea kwenye ekari moja, kinachovutia zaidi katika jitihada zake kikiwa uongezaji thamani.

Aidha, hulima njugu karanga za rangi nyeupe na nyekundu ambapo huzisindika kuwa siagi (peanut) hatua anayosema imepanua soko lake.

“Kipimo cha kilo mbili cha njugu mbichi kinagharimu Sh700, na zinapoongezwa thamani gramu 250 huuza Sh350. Hii ina maana kuwa kilo mbili za siagi zinachezea Sh2, 800,” anaelezea.


Jephline Ojwang’ akionyesha njugu karanga anazolima katika Kaunti ya Migori. PICHA|SAMMY WAWERU

Isitoshe, anadokeza kwamba huandaa supu ya njugu karanga, kinywaji ambacho kwa wengi ni nadra.

Ubunifu huo, Jephline anasema umetokana na jitihada za Rongo Livelihood Women’ Group, ambapo wamehamasishwa mbinu za kusindika (processing) bidhaa za shambani.

Lina kituo cha kukusanya mazao na pia kiwanda cha uongezaji thamani.

Mihogo, Jephline huunda kripsi na vibanzi (chips), mchicha akivuna mbegu ambazo huuzia wakulima kuendeleza uzalishaji.

Mimea asilia inasifiwa kutokana na ustahimilivu wake wa makali ya kiangazi na ukame.


Mkulima Jephline Ojwang’ pia huongeza bidhaa zake thamani, ikiwemo kuunda siagi. PICHA|SAMMY WAWERU

Aidha, Jephline alikuwa miongoni mwa wakulima waliopamba Maonyesho ya Mbegu za Kiasili na Chakula cha Tamaduni za Kiafrika 2023, Makala ya Pili, yaliyoandaliwa na muungano wa Inter-Sectoral Forum on Agrobiodiversity and Agroecology (ISFAA).

ISFAA inaleta pamoja sekta za kiserikali na za kibinafsi katika kilimo, mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, ya utafiti, na makundi ya wakulima kwa lengo la kilimo endelevu na kuboresha mazingira.

Ukumbatiaji chakula asilia, wataalamu wanasema utasaidia kuangazia gapu ya usalama wa chakula nchini na baa la njaa.

Mimea asilia, kama vile wimbi, mtama, njugu karanga, mihogo, maharagwe, mahindi ya rangi, na mboga za kienyeji inastahimili kiangazi, ukame na wadudu waharibifu na magonjwa.


Mbegu za mchicha zilizozalishwa na Jephline Ojwang’. PICHA|SAMMY WAWERU