Punda wa Lamu wapumzika kiasi mwezi wa Ramadhani
NA KALUME KAZUNGU
WAISLAMU wakiendelea na kufunga na kutekeleza ibada katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, shughuli za kazi za kawaida zimechukua mkondo mwingine kiasi, punda wa kisiwani Lamu wakipewa muda mwingi wa mapumziko.
Kinyume na siku za kawaida ambapo mara nyingi utapata punda wakibebeshwa mizigo mizito kutoka sehemu moja ya kisiwa hadi nyingine, iwe ni alfajiri na mapema au jioni kabisa, msimu huu wa Ramadhani umeshuhudia wamiliki wengi wa punda wakiwapa wanyama wao ‘break’ ambapo wanatulia tu pale nyumbani.
Tangu Ramadhani kuanza, utapata punda wengi wakiwa wamefungiwa kwenye banda au kijibaraza chao wakila na kunywa na kupumzika kwa muda wa saa kadhaa.
Wale punda ambao katika miezi ya kawaida walibeba mizigo sasa wanapumzika japo kiasi, katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Bw Suleiman Ali, mkazi na mmiliki wa punda kwenye mtaa wa Mkomani kisiwani Lamu, anasema amepunguza muda wa punda wake kufanya kazi tangu Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ulipoanza kuadhimishwa.
Kulingana na Bw Ali, punda wake kwa sasa hufanya kazi kwa muda wa saa tatu pekee.
Muda uliosalia, anawaweka punda wake kupumzika bandani na kuhakikisha mnyama huyo anakula na kutunzwa vyema.
“Mwezi huu wa Ramadhani wafaa waja kuonyesha upendo kwa viumbe, iwe ni binadamu wenzao au wanyama,” akasema Bw Ali.
Anasema haoni haja yoyote ya kumfanyisha kazi punda wake kwa muda wa saa nane kama siku za kawaida.
“Muda huo wa saa tatu za kazi kipindi hiki, ninahakikisha asubuhi ninampeleka sokoni kuchukua mboga na vyakula vingine ilhali jioni pia akibeba kuni kwa muda kidogo. Kisha anarudi kubarizi,” akasema.
Bw Abdulkadir Ahmed, mkazi wa Langoni mjini Lamu, anawasihi wamiliki wenzake wa punda kuwapa wanyama wao mazingira bora ya kuishi msimu huu wa Ramadhani.
Anasema inahuzunisha kuona wengi wa wamiliki wa punda wakiwaachilia wanyama wao kurandaranda ovyo mitaani bila ya kuwapa uangalizi wa karibu.
“Si vyema kwa mwenye punda kumthamini mnyama wake wakati akitaka kumtumia kubeba mizigo tu. Utapata punde punda anapofika nyumbani kushukisha mizigo, mwenye punda anamwachilia kujitafutia chakula, iwe ni majaani au vichakani. Lazima tumpe huyu mnyama punda mapenzi yanayofaa si kwa wakati huu wa Ramadhani pekee bali pia kila wakati. Mtunze punda akutunze,” akasema Bw Ahmed.
Naye Bi Maryam Abdallah, ambaye ni mtetezi wa haki za punda kisiwani Lamu aliwashauri fidhuli wa punda kukoma kuwapiga wanyama wao.
Bi Abdallah aliwapongeza wanaowapa punda wao muda mwingi kupumzika, hasa msimu huu wa Ramadhani, akiwataka kuendeleza hulka hiyo hata baada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
“Kwa wanaopiga na kuwadhulumu punda waache tabia hiyo. Pia kwa wale wanaowapa punda wasaa wa kubarizi wasikomee tu kwa Ramadhani. Wafanye hivyo siku zote,” akasema Bi Abdallah.
Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Kituo cha Matibabu ya Punda kisiwani Lamu, Bw Obadiah Sing’oei aliwapongeza wanaozingatia maslahi na haki za kila siku za punda.
Bw Obadiah alifafanua kuwa ili mja kuzingatiwa kama mtunzaji bora wa punda, lazima ahakikishe mnyama wake anakula na kunywa vizuri, yuko na mazingira safi ya kuishi, anatafutiwa tiba anapogonjeka, anampa uhuru wa kupumzika na kuepuka kumbebesha mnyama wake mizigo mizito kupita kiasi.
“Wako wachache wanaozingatia maslahi ya punda Lamu lakini bado changamoto ipo ya baadhi ya wamiliki kuwanyanyasa wanyama wao. Tunaendeleza hamasa za kila mara kwa wenye punda kuhusiana na umuhimu wa kuwatunza hawa wanyama wao,” akasema Bw Sing’oei.
Punda ni kiungo muhimu kwa kaunti ya Lamu, ikizingatiwa kuwa ndio njia inayotegemewa na wakazi, hasa wale wanaoishi maeneo ya visiwani kusafirisha mizigo na watu.
Lamu ina zaidi ya punda 10,000.