Hatimaye Arati amteua naibu wake
NA WYCLIFFE NYABERI
GAVANA wa Kisii Simba Arati amemteua mwenyekiti wa sasa wa Bodi ya Utumishi wa Umma katika Kaunti (CPSB), Bw Elijah Julius Obebo, kuwa naibu wake.
Uteuzi wa Bw Obebo uliwekwa wazi katika Bunge la Kaunti ya Kisii Jumatano alasiri na Spika Philip Nyanumba.
“Waheshimiwa madiwani, ninayo furaha kuwajulisha kwamba nimepata mawasiliano kutoka kwa Mheshimiwa, gavana wa Kaunti ya Kisii, Paul Simba Arati, kuhusu mteule wa nafasi ya unaibu gavana. Huku akisubiri kuidhinishwa na bunge, amemteua Bw Elijah Obebo kwenye nafasi hiyo,” Spika Nyanumba alisema.
Aliyekuwa naibu gavana Dkt Robert Monda alitimuliwa afisini wiki jana baada ya Seneti kuafiki mashtaka yote manne kama yalivyoletwa na Bunge la Kaunti ya Kisii.
Kiini cha tuhuma zilizompelekea Bw Monda kufungishwa virago ni rushwa ya Sh 800,000 kutoka kwa Denis Mokaya kwa ahadi kwamba atamsaidia apate kazi ya Umeneja wa Mauzo katika Kampuni ya Maji na Maji-taka ya Gwasco pamoja na kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa kaka yake mwenyewe, Reuben Monda, kwa kukata miti katika ardhi ya familia yao.
Maseneta hao walipiga kura kwa wingi kuunga mkono mashtaka yote manne yaliyotolewa dhidi yake.
Hayo ni pamoja na ukiukaji mkubwa wa katiba, matumizi mabaya ya ofisi, utovu wa nidhamu uliokithiri na uhalifu chini ya sheria ya kitaifa.
Kufuatia kutimuliwa kwake, Dkt Monda alifika mahakamani Jumatatu, Machi 18, 2024 kupinga uamuzi wa Seneti wa kumtimua afisini.
Hata hivyo hakupata amri yoyote kuhusiana na suala hilo, na hivyo basi, gavana huyo aliendelea na mipango ya kumtaja naibu wake ndani ya siku 14 kama ilivyoelezwa katika sheria.
Bunge la Kaunti lina siku 60 za kuhakiki mteule huyo mpya
Bw Obebo anatoka katika ukoo wa Abanyaribari kama Dkt Monda. Aliapishwa kuhudumu kama mwenyekiti wa CPSB mnamo Novemba 2023.
Ukoo wa Abanyaribari ulio na kura nyingi ulimpa Bw Arati idadi kubwa ya kura zake katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Mgawanyo wa viti vya juu vya kaunti Gusii kwa kawaida huegemea misingi ya koo.
Katika hesabu ya 2022, Gavana Arati, ambaye anatoka ukoo wa Ababasi, alimchagua Dkt Monda mgombea mwenza wake. Watu wa Abagetutu walipata useneta huku Abanchari wakipata nafasi ya Mbunge Mwakilishi wa Kike.
Pia Abamachoge huwa na kura kiasi cha haja. Nao walituzwa kiti cha Spika wa Bunge la Kaunti na Abagirango wakapata nafasi ya Katibu wa Kaunti.