Makala

Mfumo wa ‘paper mulching’ kuboresha kilimo maeneo kame

March 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SAMMY WAWERU

TEKNOLOJIA ya mtandazo (mulching) imekuwepo tangu jadi, inayojulikana ikiwa ni matumizi ya nyasi kuzuia uvukizi wa maji. 

Uvukizi, ni kupotea kwa maji kupitia miale kale ya jua.

Hata hivyo, unafahamu kuwa karatasi ngumu za nailoni zimechukua mahala pa nyasi?

Maarufu kama paper au plastic mulching, mbali na kuzuia maji kupotea shambani hasa msimu wa kiangazi (evaporation), mfumo huu unadhibiti kero ya magonjwa kwa mimea.

Shamba linaandaliwa muinuko wa vipande sawa na vitanda, kisha vinatandazwa karatasi ya nailoni.

Karatasi hiyo inajulikana kama dam liner.

Sammy Mwaniki mkulima aliyekumbatia teknolojia ya paper mulching. PICHA|SAMMY WAWERU

Hata ingawa vipimo vinategemea na mimea, pililili mboga (hoho), kwa mfano, Samuel Waikwa mtaalamu kutoka Osho Chemicals anasema kina (height) kinapaswa kuwa sentimita 30, upana semtimita (width) 36 na urefu (length) sentimita 100.

“Karatasi za nailoni ni mojawapo ya teknolojia ya kilimo hifadhi na endelevu, ambayo wakulima wanapaswa kukumbatia ili kuongeza kiwango cha mazao,” Waikwa anasema.

Hususan maeneo ha jangwani na nusu jangwa (Asal), wakulima wanahimizwa kuikumbatia, bila kusahau mashamba ya mijini ili kusaidia kuzalisha chakula.

Waikwa, anasifia mfumo wa dam liner kuangazia kero ya upungufu na ukosefu wa maji kuendeleza shughuli za kilimo.

Mkulima Sammy Mwaniki akionyesha pilipili mboga zilizokuzwa kwa kutumia karatasi ngumu ya nailoni kuzuia maji kupotea kupitia miale kali ya jua. PICHA|SAMMY WAWERU

Changamoto kuu inayozingira wakulima ni uhaba wa maji na wakikumbatia paper mulching tatizo hilo litakuwa historia, mtaalamu huyo anasisitiza.

“Kiwango cha uvukizi wa maji kinapunguzwa pakubwa,” Waikwa anasema.

Kando na kuwa faafu kwa hoho, mfumo huo pia ni bora katika uzalishaji wa stroberi, nyanya, kabichi, spinachi na sukuma wiki.

Sammy Mwaniki, mkulima wa mseto wa mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha na kukomaa – aghalabu miezi mitatu hadi sita, amekumbatia mfumo huo.

Sammy Mwaniki akikagua jinsi pilipili mboga alizolima kupitia mfumo wa paper mulching zinavyoendelea shambani mwake Gilgil, Nakuru. PICHA|SAMMY WAWERU

“Nimeshuhudia faida kibao kutokana na paper mulching,” Mwaniki anakiri.

Anaendeleza kilimo eneo la Gilgil, Kaunti ya Nakuru.

Aidha, hutumia mfumo huo kukuza pili pili mboga – maarufu kama hoho na mboga.

Mfumo huo hauhitaji mwalimu kuutekeleza.

Pilipili mboga zikiendelea kukua, ambazo zimelimwa kupitia mfumo wa paper mulching. PICHA|SAMMY WAWERU

Karatasi inapotandazwa juu, mashimo ya upanzi hutobolewa.

Katikati mwa vijitanda vya shughuli hiyo, ni mitaro inayomwagwa maji yavutwe na mimea.

“Mifereji ya kudondoa maji pia inaweza ikawekwa kwenye laini za mimea,” mtaalamu Waikwa anasema.

Mimea inayolimwa kupitia mfumo huo, inazalisha chini ya miezi miwili, mboga nazo kama vile sukuma wiki na spinachi zikichukua mwezi mmoja pekee.

Mkulima Sammy Mwaniki na mtaalamu Samuel Waikwa, akipata maelekezo kuhusu teknolojia ya paper mulching. PICHA|SAMMY WAWERU