Makala

Gachagua afichua alikuwa akibugia pombe kreti nzima

March 20th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesimulia jinsi alivyokuwa amezama kwa pombe kiasi kwamba alikuwa akibugia kati ya chupa 24 na 36 kwa kikao kimoja pekee.

“Mimi nilikuwa nimeiamulia pombe hadi wakati nilipofanya uamuzi wa busara na kuachana nayo. Katika mtaa wa Ngara kulikuwa na kilabu karibu na shule…hapo hungenitoa. Nilikuwa nakunywa kreti moja…moja na nusu, huku nikishabikia muziki wa Mugithi,” akasema Bw Gachagua.

Kreti moja ya bia huwa na chupa 24, hivyo basi kreti moja na nusu kwa ujumla ni chupa 36.

Akihutubia wanafunzi wanaosomea Chuo Kikuu cha Murang’a, Naibu Rais alisema kwamba ikiwa hangeachana na pombe, maisha yake kwa sasa yangekuwa hayana mwelekeo.

“Marafiki wangu wengi wa enzi hizo zangu za ulevi kwa sasa wameaga dunia, wengine wamegeuka kuwa ma-zombie huku wengine wakiwa wamesambaratikiwa na maisha kiasi kwamba hunitegemea niwasaidie kukidhi mahitaji yao ya kimaisha,” akasema.

Naibu Rais Rigathi Gachagua ahutubia wakulima wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kahawa eneo la Ikundu, Kaunti ya Murang’a mnamo Machi 20, 2024. PICHA | JOSEPH KANYI

Alisema kwamba ikiwa hangeachana na pombe, maisha yake yangeishia kuwa hayo tu ya marafiki wake ambao kwa sasa huishi kwa majuto makuu.

“Wewe ukiwa mwanafunzi achana na pombe kwa kuwa itakuharibia maisha. Ikiwa wewe ni shabiki wa pombe, tafadhali achana nayo. Maisha yako yatanyooka ukiwa umefanya huo uamuzi,” akashauri.

Akaongeza Bw Gachagua: “Nichukue kama mfano ambapo nimekiri kwamba nilikuwa ninakunywa pombe lakini nikaachana nayo. Angalia pale niko saa hii kimaisha. Singekuwa katika afisi hii ya Naibu Rais. Hata wewe makinikia maisha yako.”

Bw Gachagua alisema kwamba vita vyake na ulevi kiholela ni vya kulinda vizazi lakini hatafanikiwa ikiwa walengwa wa kulindwa hawatawajibikia maisha yao.

“Wewe ukiwa mwanafunzi, kwa sasa unafaa umtuze mzazi wako zawadi ya kukimbizana na yale yatakuinua kimaisha. Jali maisha yako na utie bidii. Kwa sasa mko na serikali ambayo inawajali na viongozi hawalali wakisaka suluhu ya kufanikisha maisha yenu wanafunzi na raia wengine,” akasema.

Aidha, Bw Gachagua aliwataka wanafunzi hao wamuige kwa kusema ukweli.

“Ukiwa unataka kuwa kiongozi, kuwa msema kweli na uwe muwazi. Liseme lilivyo na utaheshimika. Mimi ni shahidi kwamba ukweli hauwezi ukafunikwa. Useme jinsi ulivyo,” akasema.

Alisema kuwa utawala wa Rais William Ruto utakuwa katika mstari wa mbele kuwakinga wanafunzi dhidi ya madhara na pia kuwaimarishia nafasi za kuafikia malengo yao ya kimaisha kupitia sera thabiti.