Straika 'tineja' alishwa marufuku baada ya kubainika ana miaka 28
Na GEOFFREY ANENE
MFUNGAJI mwenye umri mdogo kuwahi kushuhudiwa katika Ligi Kuu ya Soka ya India amepigwa marufuku miezi sita baada ya kugunduliwa alikuwa karibu maradufu ya umri wake.
Mwezi Oktoba mwaka 2018, mvamizi wa Jamshedpur FC, Gourav Mukhi alipachika bao la kusawazishia timu yake ilipotoka 2-2 dhidi ya Bengaluru FC.
Lilikuwa tukio la kihistoria Mukhi aliyekuwa ameorodheshwa kama chipukizi wa miaka 16 alipopokea zawadi ya mfungaji wa kwanza kabisa mwenye umri mdogo katika ligi hiyo maarufu kama ISL.
Alipongezwa hata uwanjani na mchezaji mwenza Tim Cahill, ambaye ni mfungaji bora wa timu ya taifa ya Australia. Aliambia “tineja” huyo, “Huu ni wakati wako mzuri kabisa maishani mwako.”
Hata hivyo, mambo yaligeuka haraka na kuwa mabaya kwake pale masharubu aliyokuwa nayo yalipoanza kumfanya watu walitie shaka umri wake.
Mukhi sasa amepigwa marufuku miezi sita na pia usajili wake kufutiliwa mbali na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka la India (AIFF) aliposhindwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha umri wake.
Inasemekana Mukhi alisajiliwa na klabu hiyo kama mchezaji mwenye umri wa miaka 16. Mbali na masharubu yake, ukurasa wake waFacebook pia ulikanganya watu kwa sababu unasema alizaliwa Aprili 5 mwaka 1999.
Nalo gazeti la Telegraph of India lilichapisha habari kumhusu mwezi Septemba iliyosema kwamba ana umri wa miaka 28.