Juhudi za Kalonzo kujivua ‘mikosi’ ya Raila
NA BENSON MATHEKA
JUHUDI za sasa za kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kupigia debe azma yake ya urais kivyake ni kutaka kujitoa kutoka mbawa za kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga ambaye wameshirikiana kisiasa tangu 2013.
Wadadisi wanasema kwamba kwa kufanya hivi, Bw Musyoka anataka kuonyesha anaweza kujimudu kisiasa bila kumtegemea kigogo huyo wa siasa za upinzani mwenye umaarufu mkubwa kote nchini.
Japo chama chake kingali katika muungano wa Azimio, Bw Musyoka ameungana na mwenzake wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa kuunda mrengo anaotumia kujipigia debe kama mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Mrengo wake umevutia baadhi ya vinara wenza wa muungano huo Peter Munya wa chama cha PNU na Mwangi wa Iria wa Usawa Civic Party na wamekuwa wakifanya kampeni maeneo tofauti bila kushirikiana na Bw Odinga na chama chake cha ODM ambacho ndicho kikubwa katika muungano huo.
Bw Musyoka na washirika wake wamekuwa wakisisitiza kuwa Odinga anafaa kurudisha mkono na kumuunga makamu rais huyo wa zamani ambaye hajamuacha tangu 2013 walipogombea urais pamoja chini ya uliokuwa muungano wa Coalition For Restoration of Democracy (CORD) hadi 2022 walipokuwa pamoja katika muungano wa Azimio.
Katika chaguzi hizo tatu hawajawahi kufaulu kuunda serikali. Bw Odinga na washirika wake wamekuwa wakidai kwamba hajawahi kuingia ikulu na hivyo kupuuza wito wa kumuunga mkono Bw Musyoka. Shinikizo za waziri mkuu huyo wa zamani kumuunga Musyoka 2027 zimezidi baada ya kutangaza azima yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika AUC na kuibuka uwezekano wake kutokuwa kwenye debe katika uchaguzi mkuu ujao.
Wadadisi wa siasa wanasema kwamba juhudi za sasa za Bw Musyoka zinalenga kumsawiri kama mwanasiasa mwenye uwezo wa kugombea urais kivyake bila kutegemea kuidhinishwa na Odinga kama mrithi wake.
“ Hataki kurithi mikosi ya Odinga ya kutoshinda urais mara tano. Hataki kuonekana kama anayetegemea vigogo wengine kumpigia debe na hii ni hatua nzuri hasa wakati huu ambao kuna dalili za kiongozi huyo wa ODM kutoshiriki kikamilifu siasa za Kenya au kugeuza mkondo na kuwa na washirika wapya ifikapo 2027,” asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.
Anasema juhudi za Bw Musyoka zinaweza kumshindia mtandao wa washirika kutoka maeneo tofauti badala ya kutegemea Odinga.
“ Ukweli ni kwamba akiungwa mkono na Odinga, anaweza “kurithi” kura za eneo la Nyanza. Hata hivyo, Odinga amejivuta kumuidhinisha ishara kwamba kuna shinikizo asifanye hivyo kutoka kwa washirika wa ngome yake ya Nyanza wanaonufaika na jina lake au kwingineko, ikiwemo mikakati ya kubadilisha mkondo wa siasa akishinda au asiposhinda kiti anachowania AUC,” asema Gichuki.
Mdadisi wa siasa Brian Khatete, anasema juhudi za Musyoka za kujiandaa kivyake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 zitamsaidia kujitakasa na shutuma kwamba anategemea kutangazwa tosha na Odinga.
“Bw Odinga anabebeshwa nembo ya kushindwa katika azma ya urais licha ya kuwa na umaarufu mkubwa. Japo huwa analalamika kuibiwa ushindi, ukweli ni kwamba Bw Musyoka hana budi kujitakasa na mkosi huo kwa kuepuka makosa ambayo Bw Odinga huwa anafanya,” asema.
Wiki hii, Bw Musyoka alizuru eneo la Nyanza ngome za ODM kupigia debe azima yake ambapo aliapa kuwa atatoshea katika viata vya Odinga iwapo azma ya AUC itafaulu.
Katika ziara hiyo Kisii, Nyamira na Migori alijisawiri kama mwanasiasa mwenye uzoefu na sifa za kutosha kuwa rais.
Alitangulia eneo la Mlima Kenya Mashariki na anapanga kuzuru eneo la Kati na Pwani.