Lugha, Fasihi na Elimu

Prof Mukoma wa Ngugi: Kufunguka mateso aliyopitia mama kunanipa nguvu

March 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

PROFESA Mukoma wa Ngugi, anayetambulika kwa fani ya Fasihi alisema wiki iliyopita kwamba kimya kuhusu hali ya mamake ‘kudhulumiwa’ kwa ndoa kimekuwa kikimwathiri vibaya hivyo akaona ni heri atoe ya moyoni.

Alisema kuweka mambo wazi kumemletea utulivu licha ya kushambuliwa kimaneno.

Yeye ni mwanawe Prof Ngugi wa Thiong’o, mwandishi shupavu wa vitabu.

Prof Mukoma alisisitiza hatabadilisha kauli kwamba marehemu mamake, Bi Nyambura wa Ngugi alikuwa akipitia dhuluma za kinyumbani.

Msomi huyo alitoa kauli hiyo wiki iliyopita, hali ambayo imezua hisia kali miongoni mwa marafiki na mashabiki wa msomi na mwandishi huyo maarufu kote duniani, anayehudumu kama Mhadhiri wa Fasihi katika Chuo Kikuu cha California, Irvine, Amerika.

“… Marehemu mamangu [Nyambura] alikipitia na baadhi ya kumbukumbu zangu za utotoni ni kwamba ningeenda kumtembelea kwa nyanyangu, alikokuwa akitorokea kuepuka dhuluma. Hata hivyo, kile hunisumbua ni kimya kuhusu masaibu yake. Basi, nimesema hayo,” akasema Prof Mukoma, kwenye ujumbe alioandika katika mitandao ya kijamii.

Wiki moja baada ya kuandika ujumbe huo, na huku kauli hiyo ikiendelea kuzua mjadala katika majukwaa mbalimbali ya kiusomi, Prof Mukoma anasisitiza kuwa hatabadilisha kauli yake licha ya shinikizo na ukosoaji mkubwa ambao umekuwa ukielekezwa kwake.

Lakini anasema asieleweke vibaya na hana ubaya na babake au mtu mwingine yeyote wa familia.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo kwa njia ya simu kutoka nchini Amerika mnamo Jumatano, Prof Mukoma alisema hatabadilisha msimamo wake hata kidogo kwani “ukweli kamwe hauwezi ukafutika”.

“Ukweli kamwe hauwezi ukabadilika, iwe msema ukweli atapigwa au la. Ukweli haubadiliki,” akasema bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Prof Mukoma pia alikiri kutengwa na kukasirikiwa na baadhi ya jamaa zake kutokana na kauli hiyo.

“Ninaelewa sababu ambapo jamaa zangu wamekasirishwa na kauli niliyotoa kumhusu babangu. Sijali, hata ikiwa nilitoa kauli hii bila ruhusa kutoka kwao. Hali ni kama hiyo kwa marafiki na wasomi ambao ni marafiki wa karibu wa babangu. Kile sitajali ni kauli za baadhi ya watu kwamba nilieleza uwongo,” akasema.

Hata hivyo, mnamo Jumatano, wanawe msomi huyo–Nducu wa Ngugi, Wanjiku wa Ngugi na Njooki wa Ngugi–walionekana kupuuzilia mbali madai ya ndugu yao mkubwa, kwa kuweka picha wakiwa pamoja na Prof Ngugi.

Prof Ngugi alihamia nchini Amerika katika miaka ya 1980, baada ya kuhangaishwa kisiasa na serikali za marais Hayati Mzee Jomo Kenyatta na marehemu Daniel Moi.

Mbali na suala la marehemu Nyambura, familia ya Ngugi imekuwa ikiishi kwa upendo mkubwa ambapo Prof Ngugi na Prof Mukoma wamekuwa wakitoa mihadhara katika taasisi tofauti za elimu ya juu katika sehemu mbalimbali duniani.

Mnamo 2015, wawili hao walitoa mihadhara katika vyuo vikuu kadhaa nchini, kama vile Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), ambako Ngugi alihudumu kama mhadhiri wa fasihi kabla ya kukamatwa kutokana na vitabu vyake vilivyoonekana kuikashifu serikali ya Mzee Jomo Kenyatta.

Pia Prof Ngugi na Prof Mukoma walifanya mdahalo wa pamoja wa Fasihi katika Chuo Kikuu cha St Paul’s mjini Limuru, Kaunti ya Kiambu mnamo Februari 21, 2019.

Prof Ngugi alirejea nchini Kenya mnamo 2004 baada ya kukaa uhamishoni nchini Amerika kwa karibu miaka 22.

Msomi huyo alikuwa ametoroka nchini baada ya kuandika vitabu vyenye jumbe za kisiasa kama ‘Ngaahika Ndeenda’ (Nitaoa Nikipenda) na ‘Caitaani Mutharaba-ini’ (Sherani Msalabani) vilivyozilaani serikali za marais Moi na Kenyatta.

Kwa miaka kadhaa iliyopita, Prof Ngugi amekuwa miongoni mwa waandishi ambao wamekuwa wakipigiwa upatu kushinda tuzo ya Nobel kutokana na umahiri wake mkubwa katika uandishi wa vitabu.

Amekuwa akizuru katika maeneo tofauti duniani akitoa mihadhara kuhusu historia, fasihi, demokrasia, sanaa, haki za binadamu miongoni mwa masuala mengine ya kiusomi na uandishi kwa upana.