Habari za Kitaifa

Jinsi mhasibu alivyozamisha Sh16m kwa shamba hewa

March 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MHASIBU anayeishi ng’ambo alitapeliwa zaidi ya Sh16 milioni kwa kuuziwa shamba hewa jijini Nairobi, hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bi Susan Shitubi amefahamishwa na polisi.

Akitoa ushahidi dhidi ya Stephen Njoroge Mbugua anayeshtakiwa kumlaghai Bw Joseph Gitau, Inspekta Benjamin Chelang’a aliwasilisha taarifa za benki kuhusu ununuzi huo wa shamba katika mtaa wa kifahari wa Karen jijini Nairobi.

Hakimu Shitubi alielezwa Mbugua alitumiwa pesa kutoka New York kumnunulia shamba Gitau lakini “hakununua.”

Bw Chelang’a alisema alienda katika benki ya Equity kufanya uchunguzi na alipopata taarifa za benki, aligundua mshtakiwa (Njoroge) alipokea pesa hizo katika akaunti ya Dola (USD).

Afisa huyo alimkabidhi Bi Shitubi nakala hizo pamoja na jumbe za mawasiliano kwa mtandao wa WhatsApp.

Akionyesha mawasiliano hao, Bw Chelang’a alisema ujumlishaji wa ushahidi huo umeonyesha kabisa Njoroge alipokea pesa kutoka kwa Bw Gitau.

Hakimu alifahamishwa kwamba mshtakiwa aliweka tangazo katika vyombo vya habari kuhusu ploti za kuuza mtaani Karen.

“Bw Gitau alisafiri kutoka New York akiandamana na mkewe kumtembelea Njoroge ili awapeleke katika ploti hizo alizokuwa ametangaza zinauzwa,” Bw Chelang’a alisema.

Mahakama ilielezwa Bw Gitau alitembezwa tu kule Karen lakini hakuonyeshwa ploti yake.

Bi Shitubi alifahamishwa na Bw Gitau anayeishi nchini Uingereza sasa kwamba alishtuka Njoroge alipomweleza aliugua ugonjwa wa Ndui (smallpox) kisha akasafiri kutibiwa ng’ambo.

Wakili Robert Asembo anayemwakilisha Bw Gitau aliomba mahakama imtendee haki mlalamishi ikitiliwa maanani alitapeliwa na kupoteza pesa zake.

Bw Asembo alieleza mahakama ni miaka saba tangu mlalamishi auziwe ‘ploti hewa’ na haki inastahili kutekelezwa.

Bw Gitau alieleza mahakama kwamba mnamo Oktoba 1 2017, alimtumia Njoroge pesa na kuzipokea katika akaunti yake iliyoko Benki ya Equity tawi la Karen.

Njoroge alithibitisha alipokea pesa hizo kutoka Benki ya New York.

Pia hakimu alifahamishwa mshtakiwa alisafiri hadi Ufilipino alikoenda kutibiwa maradhi hayo ya Ndui.

Bw Gitau alisafiri kutoka New York hadi Nairobi kuonyeshwa ardhi aliyonunuliwa lakini kile alionyeshwa tu “ni matangazo katika vyombo vya habari ya ardhi ya nusu ekari zilizokuwa zinauzwa. Hakuna ardhi aliyoonyeshwa.”

Bw Chelang’a aliwasilisha kortini mkataba wa mauzo ya shamba kati ya Bw Gitau na Bw Njoroge katika mtaa wa Karen.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Mei 2, 2024.

Mshtakiwa amekanusha mashtaka dhidi yake na yuko nje kwa dhamana.