Staa wa Brazil, Robinho atupwa jela miaka tisa kwa tamaa ya visketi
IMEKUSANYWA NA CHRIS ADUNGO
ALIYEKUWA fowadi wa Manchester City na timu ya taifa ya Brazil, Robson de Souza almaarufu Robinho, hatimaye ataanza kifungo cha miaka tisa gerezani kwa kuwa kati ya wanaume waliombaka mwanamke kwa zamu nchini Italia, mahakama ya Brazil imeamua.
Ingawa Italia ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Robinho, nyota huyo wa zamani wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alikwepa jela kwa miaka saba akiishi Sao Paulo, Brazil.
Alipatikana na hatia hiyo ya ubakaji mnamo 2017 na sasa atatumikia kifungo chake nchini Brazil kwa ombi la mamlaka za Italia, katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa.
Japo mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Santos nchini Brazil alisisitiza hana hatia, Mahakama ya Juu ya Haki nchini Brazil (STJ) iliingilia ombi la Italia kutaka atumikie kifungo.
Majaji tisa kati ya 15 walipiga kura ya kuunga mkono amri ya Robinho kutumikia kifungo nchini mwake, katika uamuzi wa hatima ya staa huyo aliye sasa na umri wa miaka 40.
Majaji hao wa STJ hawakumhukumu upya Robinho, ila walipiga tu kura ya kuamua iwapo anastahili kutumikia kufungo nchini Brazil au la.
Sogora huyo mstaafu aliyehukumiwa Italia, anatazamiwa sasa kufungwa mara moja kwa mujibu wa ripoti ya mtandao wa Globo.
Robinho alikuwa miongoni mwa wanaume sita waliopatikana na hatia ya kubaka na kumdhulumu kimapenzi mwanamke raia wa Albania mnamo Januari 22, 2013, akiwa bado mchezaji wa AC Milan nchini Italia.
Mahakama ya Italia ilimpata na hatia hiyo Novemba 2017 na amekuwa akijaribu mara kadha kukata rufaa bila mafanikio.
Robinho kwa sasa anaishi Sao Paulo, Brazil, na alisalimisha stakabadhi zake za usafiri kwa mamlaka za nchi yake mnamo Machi 2023 baada ya kifungo chake kuidhinishwa 2022.
Robinho ameshikilia kuwa hana hatia na kusisitiza kisa cha ubakaji cha 2013 kinachorejelewa ni tukio alilofanya kwa makubaliano na mwathiriwa.
Sogora huyo amewahi pia kusakatia Real Madrid ya Uhispania. Alitia saini mkataba wa mwaka mmoja mnamo 2020 kuchezea kikosi chake cha awali cha Santos.
Kwa mujibu wa sheria za Italia, hukumu yake haitaanza hadi mchakato mzima wa kukata rufaa ukamilike.
Katiba ya Brazil hairuhusu raia wa taifa hilo waliohukumiwa ugenini kurejeshwa nchini. Hiyo inaamanisha kuwa hadi leo, Robinho angeweza tu kukamatwa ikiwa angesafiri nje ya nchi.
Mnamo Novemba 2023, waendesha mashtaka wa Italia walisema walihisi Robinho alifaa kutumikia kifungo chake nchini Brazil.
Awali kabisa, Brazil nayo ilisema kuwa sogora huyo alistahili kufungwa nchini Italia, ikisisitiza kuwa hatua hiyo ingewakilisha juhudi za pamoja za mahakama kushirikiana ili kukabiliana na uhalifu.
Robinho ameshutumu mfumo wa haki nchini Italia kutawaliwa na “ubaguzi wa rangi”.