MUTUA: Serikali itukinge dhidi ya wadukuzi katika mitandao
MPENZI wa TikTok utafanyaje ukiamka asubuhi moja upate mtandao huo haupo tena, hivyo huwezi kurekodi video za nyimbo na vichekesho, wala huwezi kuziona zozote zilizorekodiwa na kupakiwa huko na marafiki zako au watu mashuhuri unaofuata?
Utakwenda kushtakia hali kwa nani au utasubiri mafundi wakutengenezee mtandao, wakishindwa ukubali yaishe, ujipe shughuli kwa mambo mengine muhimu na yenye tija? Hivi una uwezo gani wa kuwawajibisha wamiliki wa mtandao huo kuhakikisha unapata huduma hiyo bila kuikosa, tena hawatumii vibaya taarifa zinazokuhusu, hasa kuhujumu usalama wa taifa?
Labda Mkenya wa kawaida hajali kuhusu usalama wa taifa, hasa kwa kuwa tunaichukulia hiyo kama kazi ya serikali, lakini atashtuka akisikia nambari yake ya simu au anwani ya baruapepe imetumiwa na wakora wanaodukua mitando kujinufaisha.
Mojawapo ya maswali makuu ambayo nimejiuliza ni: Je, Kenya ina mtetezi katika masuala changamano ya dijitali au tumeachiwa Mungu, wadukuzi wafanye nasi wanavyotaka?
Nimesalitika kujiuliza swali hili baada ya kushuhudia wabunge wa Amerika wakitishia kuipiga marufuku TikTok iwapo anayeimiliki hatakubali kuiuzia Amerika.
Mwanzoni, nilijiuliza tunaishi katika ulimwengu gani ambapo taifa hilo tajiri na lenye nguvu zaidi duniani linaweza kumlazimisha mtu binafsi kuuza biashara yake, lau sivyo apokonywe au ifungwe kama kibanda cha kuuzia mchicha.
Amerika imejua kuwa ujasusi wa kimataifa umepanda ngazi pakubwa, nchi zinaacha kutumia watu kwa kiasi kikubwa kuchunguza nchi za watu, shughuli hiyo muhimu ya usalama wa taifa ikihamia mtandaoni.
Kwa kutambua kuwa ujasusi umeingia kwenye enzi ya dijitali, Amerika iko sahihi kwa kuwa serikali zilizoendelea zimeajiri wadukuzi rasmi, na zinawatumia kwa wepesi kila zikitaka kulemazana.
Hata nchini Kenya nina hakika umewahi kusikia kuwa baadhi ya wizara au idara za serikali zimeingiliwa mtandaoni ikawa kwamba, hakuna shughuli zinazoweza kuendelea.
Benki Kuu ya Kenya imewahi kuibiwa mamilioni ya pesa na wajanja wetu kwa njia hiyo. Hilo ni mojawapo ya aina za mashambulizi yaliyotekelezwa na Urusi dhidi ya Ukraine nchi hizo zilipoanza vita miaka miwili iliyopita.
Amerika pia imewahi kushambuliwa.
Wakenya, kama watu wanaotumia teknolojia ya dijitali kwa kiwango kikubwa, wanapaswa kuishurutisha serikali yao kubuni mikakati ya kuwaweka salama dhidi ya uvamizi wa kidijitali kutoka nje ya nchi.