MUSYOKI: Serikali ya Kenya Kwanza ionyeshe nia njema kwa sekta ya elimu nchini
SIKU tatu zilizopita, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo (Kuppet) Akelo Misori, alitishia kuongoza walimu kushiriki mgomo ikiwa serikali haitatuma Sh54 bilioni ambazo taasisi hizo zinaidai kabla ya muhula wa pili kuanza Aprili 29, 2024.
Kuppet ilichukua hatua hiyo baada ya katibu wa Elimu Msingi, Belio Kipsang kutangaza kuwa, serikali itatuma Sh6.25 bilioni wiki mbili zilizofuata kuanzia Jumatano iliyopita bila kurejelea kiasi ambacho chama hicho kilitaja.
Ikiwa zimeasalia wiki mbili tu shule zifungwe Aprili 5, 2024, ni bayana kuwa wasimamizi wa shule wamepitia wakati mgumu kuendesha shughuli za masomo bila ufadhili huo.
Hii si mara ya kwanza serikali kuchelewesha hela hizo licha ya Waziri wa Elimu, Ezekiel Machogu kutoa ahadi na hakikisho mara kwa mara.
Mbali na kuwawia kwa ufadhili, serikali imepunguza kiwango cha mgao wa pesa kwa kila mwanafunzi kwa mwaka kutoka Sh22,244 hadi Sh17,000, jambo ambalo limeshangaza maafisa wa Kuppet waliotarajia uongezwe kutokana na gharama ya juu ya maisha.
Aidha, Wizara ya Elimu imekatiza ufadhili wa huduma ya matibabu ya wanafunzi kupitia bima ya Edu-Afya kuanzia Januari 2024 bila kutoa afueni mbadala kulingana na Mwenyekiti wa Kuppet, Omboko Milemba.
Ilipoingia mamlakani, serikali ya Kenya Kwanza iliahidi kuinua viwango vya elimu kupitia ukuzaji wa Mtaala mpya wa Utendaji na Umilisi (CBC) ambao uliasisiwa na uongozi uliotangulia.
Hata hivyo, mabadiliko yaliyotekelezwa ya kuweka Shule za Sekondari ya Chini (JSS) kwenye usimamizi wa shule za msingi haujaonekana kuzaa matunda kufikia sasa.
Mfumo huo mpya umekumbwa na dosari kadha wa kadha ukiwepo upungufu mkubwa wa walimu na vifaa, ambapo shule za mashambani zimeathirika zaidi.