Wataalamu wataja hatari za uuzaji wa mbolea bandia
NA BENSON MATHEKA
USAMBAZAJI wa mbolea bandia kupitia shirika la serikali, umeibua hofu kuhusu mipango ya watu wenye ushawishi wanaotaka kupalilia umaskini na njaa nchini na kuua uchumi wa wakulima.
Wataalamu wa kilimo wanasema kwamba kusambazwa kwa mbolea hiyo bandia kupitia Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) ni ushahidi tosha kwamba kuna njama pana ya kulemaza uchumi wa wakulima na kuvuruga juhudi za nchi kujitosheleza kwa chakula.
Mnamo Jumamosi, Machi 23, 2024 maafisa wa usalama walinasa magunia 560 ya mbolea bandia iliyotarajiwa kuuziwa wakulima katika Kaunti ya Nakuru.
Hi ni baada ya maafisa hao kupata ripoti za ujasusi mnamo Jumamosi kuhusu uwepo wa bidhaa hiyo katika ghala la NCPB.
Kinachoibua maswali na hofu, ni nani alikubali shehena hiyo ya mbolea kuhifadhiwa katikaa ghala la NCPB hata baada ya agizo kutoka kwa Katibu wa Wizara ya Kilimo Dkt Paul Ronoh isikubaliwe kuhifadhiwa.
Duru zilisema kuwa shehena hiyo ya mbolea (magunia 560) iliwasilishwa katika ghala la NCPB, Molo licha ya barua kutoka kwa Dkt Ronoh kuagiza izuiwe.
Katika barua aliyotuma mnamo Machi 20, 2024, Katibu Ronoh alisema kuwa mbolea hiyo haijaafikia viwango vinavyohitajika.
Kulingana na mbunge wa Gem David Ochieng, inasikitisha Wakenya wamekuwa wakiuziwa mbegu na mbolea bandia.
Alihusisha sakata hii na ufisadi katika sekta ya kilimo akisema iwapo hatua hazitachukuliwa kuuzima, itakuwa vigumu kuafikia utoshelevu wa chakula nchini.
“Suala la ufisadi katika kilimo limekuwa donda ndugu na ni lazima tukabiliane nalo kama nchi. Lazima tukabiliane na chanzo cha tatizo hili na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo bora,” alisema akiwa eneobunge lake mnamo Jumamosi.
Mtaalamu wa Kilimo Deborah Weru anasema matumizi ya mbolea duni yananyima wakulima mavuno na kuwasababishia hasara.
“Kuna hatari nyingi za kutumia pembejeo duni za kilimo. Moja, ni wakulima kupata hasara kwa kukosa mavuno mazuri. Pili, ni nchi kushindwa kulisha raia wake kwa kutumia chakula kinachozalishwa nchini, na tatu, ni kuua uchumi wa eneo linalotegemea kilimo,” asema.
Mtaalamu huyu anasema sakata kama hiyo haiwezi kufanyika bila kuhusika kwa watu walio na ushawishi serikalini.
“Sio suala ndogo baadhi ya watu wanavyofikiria. Mfanyabiashara wa kawaida hawezi kuamka na kuagiza mbolea. Ni biashara inayohusisha idara kadhaa za serikali na lazima wanaohusika ni watu walio na ushawishi mkubwa,” asema.
Uuzaji wa mbolea na mbegu bandia ni hatari kwa usalama wa taifa kwa kuwa unaweza kusababisha uhaba wa chakula.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi Bw Stephen Musimbi anasema wanaohusika ni watu wanaofaidika na tenda za kuingiza chakula nchini kukiwa na uhaba wa chakula.
“Ni mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wenye ushawishi na matokeo yake ni kuwa itakuwa mlima kwa nchi kukuza chakula cha kutosheleza raia wake,” asema.