Habari za Kaunti

Baa zote zafungwa licha ya korti kuagiza zifunguliwe

March 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GITONGA MARETE NA STEPHEN MUNYIRI

MJI wa Karatina Kaunti ya Nyeri, hauna baa yoyote inayohudumu baada ya serikali kufunga baada zote katika juhudi za kukabiliana na ulevi wa kupindukia.

Baa na maduka 300 ya kuuza pombe na vileo zilifungwa katika operesheni iliyochukua wiki moja, huku maafisa wa serikali wakisema zilikuwa karibu na taasisi za masomo na makanisa.

Baa saba zilizonusurika msako huo zilifungwa Ijumaa (Machi 22, 2024) huku wafanyabiashara wakidai kuna ubaguzi katika utekelezaji wa kanuni mpya za kudhibiti uuzaji wa pombe.

Haya yanajiri huku maafisa wa serikali wakikaidi agizo lililotolewa na korti wiki jana kuruhusu wamiliki wa baa kuzifungua baada ya kuomba mahakama kubatilisha hatua ya serikali ya kuondoa leseni zao.

Lakini Naibu Rais Rigathi Gachagua alisisitiza kuwa serikali haitalegeza kamba katika vita dhidi ya utengenezaji wa vileo na akaonya wamiliki wa baa aliosema wanapigana na serikali kujiandaa kwa vita vikali.

“Hatuwezi kuruhusu watoto wetu kunywa sumu. Baadhi ya watu wanataka tulegeze kamba katika vita hivi lakini tutaendelea kwa sababu tunajali watu wa Kenya. Nitakuwa mjinga iwapo nitaruhusu watu wangu kuuawa na pombe na dawa za kulevya,” Bw Gachagua alisema akiwa katika shule ya sekondari ya Abothuguchi, Imenti ya Kati, Kaunti ya Meru.

Naibu Rais alizindua oparesheni kukabiliana na kero ya pombe haramu na hatari, na dawa za kulevya mapema 2023.