Makala

Mwanaharakati atoka mafichoni kuendelea kutetea maskini

March 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA BENSON MATHEKA 

ALITOROKEA Iceland, alikoishi uhamishoni kwa miaka minne na sasa amerudi Kenya kuendeleza shughuli zake za uanaharakati nchini.

Alilazimika kuondoka Kenya akidai kwamba maisha yake yalikuwa hatarini kwa sababu ya kutetea haki za maskini.

Juzi, alichangia kuzima kubadilishwa kwa fimbo ya mamlaka ya bunge kwa anachotaja kuwa njia ya kiholela.

David Kimengere Waititu alikuwa akiongoza watu wa familia kuzuia ardhi yao kunyakuliwa na watu walio na ushawishi, baadhi yao mabwanyenye na maafisa wa serikali.

Katika eneobunge la Othaya, Kaunti ya Nyeri alikozaliwa, anafahamika kama Sauti ya Mnyonge kwa sababu ya kutetea haki za akina yakhe.

 “Siwezi kunyamaza ndugu na dada zangu nchini wakiendelea kunyanyaswa na mabwanyenye na wanasiasa. Nitaendelea kufanya kila niwezavyo kuhakikisha haki zao zinaheshimiwa kupitia utawala bora, uwazi na uwajibikaji,” Kimengere aliambia Taifa Dijitali.

Akiwa uhamishoni, alikuwa akifuatilia kwa makini yanayotendeka nchini na kutumia mitandao kuhimiza Wakenya wasivunjike moyo bali waungane kutetea na kulinda haki zao.

David Kimengere akiwa na mwanaharakati Koigi wa Wamwere. PICH|BENSON MATHEKA

“Nimesajili shirika langu kwa jina Kuungana, Kujenga Kenya kwa lengo la kuunganisha akina yakhe wazungumze na sauti moja. Hii ni baada ya kugundua kwamba wanasiasa wamekuwa wakiwagawanya kwa misingi ya kikabila ili wasiwe na nguvu za kutetea haki zao,” asema Kimengere.

Kimengere, 44, ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Kihome, Othaya kaunti ya Nyeri alianza shughuli za uanaharakati akiwa mchuuzi mjini Nyeri.

Alijiunga na siasa ili kupata nafasi ya kutetea haki za maskini kwa kugombea kiti cha ubunge cha Othaya lakini hakufua dafu.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2013, alikamatwa kwa madai ya kukiuka kanuni za uchaguzi, hatua ambayo anasema ilichochewa na wapinzani wake waliohisi kwamba akiwa mtoto wa maskini, hakufaa kushindana nao.

Bw Kimengere anasema kwamba maskini nchini wanateseka kwa sababu hawapati nafasi za uongozi zinazochukuliwa kuwa za watu wa tabaka la juu.

“Maskini nchini Kenya wanachukuliwa kama watumwa wa wanasiasa na mimi nimejitolea kujaza pengo kwa kuwaunganisha wafungue macho. Kenya sio ya familia chache zinazopora pesa za umma na kuzitumia kwa kampeni za uchaguzi mkuu,” asema.

Mwanaharakati huyu anasema aliondoka nchini baada ya kutishiwa maisha na watu wenye ushawishi alipowasilisha kesi kadhaa kupinga juhudi zao za kunyakua ardhi ya maskini.

“Sitataja watu hao kwa kuwa kesi zingali kortini,” asema.

“Nililazimika kuacha familia yangu Kenya nilipopashwa habari kwamba kulikuwa na njama ya kunidhuru kwa sababu watu fulani hawakufurahia juhudi zangu kuhakikisha maskini wanapata haki yao,” asema baba huyo wa watoto watatu.

David Kimengere Sauti ya Mnyonge Roho Safi. PICH|BENSON MATHEKA

Mbali na kupiga vita unyakuzi wa ardhi, Bw Kimengere pia anahakikisha kuwa raia wanaelewa haki zao kama wapigakura ili waweze kufanya maamuzi ya busara wakati wa uchaguzi.

“Kuna pengo kubwa kwa sababu wanasiasa wakuu hawataki maskini wajue haki zao. Hii ndio sababu elimu ya jamii kuhusu uchaguzi haitekelezwi ipaswavyo kabla ya uchaguzi mkuu na ikifanyika huwa inalenga kuwagawanya Wakenya na kuwafanya wapigane,” asema.

Anatoa mfano wa mchakato wa kubadilisha katiba ambao anasema umegawanya Wakenya kwa misingi ya kimaeneo na kijamii, japo ulidaiwa kuwa wa kuwaunganisha.

Bw Kimengere anasema kwamba hakuna kitakachomzuia kutetea haki za maskini.

“Mimi ni hasla wa kweli. Ninajua uchungu na mateso ya akina yakhe na ninahisi nikiungana na wenzangu ambao wanajali nchi yao bila tamaa, siku moja tutabadilisha mwelekeo wa demokrasia ya Kenya,” asema.

Anakanusha madai kwamba alienda Iceland kutafuta pesa za kufadhili shughuli zake za uanaharakati akisema shirika analofanya kazi nalo halina ufadhili wowote kutoka nje ya nchi.

“Nilienda Iceland kama mkimbizi kuokoa maisha yangu na sio kutafuta misaada. Ni mkimbizi gani aliye na uhuru wa kutembelea ofisi za mashirika kuomba pesa za kuendeleza uanaharakati katika nchi aliyoacha wazazi na jamaa zake anaowapenda?” anahoji.

Katika eneobunge la Othaya, anafahamika kama Sauti ya Mnyonge Roho Safi kwa sababu ya kujitolea kwake kutetea haki za maskini.

“Kimengere ni mtu roho safi sana na hataki kuona mtu akidhulumiwa,” asema James Kamuiru, mhudumu wa matatu mjini Othaya.

“Ninajua siku moja Kenya itakuwa nchi ya haki kwa raia wake wote.Mungu anaipenda Kenya na hataiacha iangamizwe na utawala mbaya,” asema.