Makala

Habida: Ilinigharimu Sh500, 000 kufanya upasuaji wa koo

March 25th, 2024 1 min read

NA SINDA MATIKO
MWANAMUZIKI Habida Moloney amefichua kuwa oparesheni ya koo aliyofanyiwa mwezi uliopita (Februari 2024) India,  kuondoa uvimbe kwenye koromeo lake ilimdona kiasi kisichopungua nusu milioni.

Februari, staa huyo alisafiri hadi India kwa ajili ya oparesheni hiyo spesheli anayosema bila hiyo, alikuwa amepoteza tayari uwezo wake wa kuimba kabisa.

Tayari amepona kiasi cha kuweza kuzungumza vyema lakini bado hajaweza kuimba.

“Sababu ya kwenda India ni kutokana na ushauri niliopata kutoka kwa daktari Mkenya. Kwa sababu ilikuwa ni oparesheni spesheli, nilishauriwa kwenda kukutana na daktari ambaye sio tu mpasuaji wa koo, lakini anayeshughulika na upasuaji wa kurekebisha kodi za sauti,” Habida anasema.

Upasuaji huo uliochukua muda wa saa nzima, ulimwacha Habida akiwa hawezi kuongea kwa siku saba.

“Teknolojia ya kisasa ilitumika ambapo ulikuwa ni upasuaji uliotumia miale ya laser. Gharama zake hazikupungua Sh500, 000 ukiachia mbali nauli za tiketi ya ndege, na gharama za hotelini,” anasema.
Kwa sasa, Habida anaendelea na mazoezi ya kujifunza kujua kuimba tena.