Makala

Pasta Ezekiel Odero alivyotatizika kwa kukosa nguvu za kiume

March 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA SINDA MATIKO

MUHUBIRI tajika Ezekiel Odero amefichua namna alivyohangaika na kukosa nguvu za kiume kwa zaidi ya miaka mitano.
Akihubiria baadhi ya waumini kwenye mkutano wake wa siku chache zilizopita kule Tanzania, muhubiri huyo alisimulia namna alivyohangaika sana kupata mtoto.

Kando na kukiri kwamba hakuwa na nguvu za uume, mke wake naye vile vile alikuwa na tatizo la kizazi jambo ambalo liliwapa wakati mgumu sana kuja kuwapata watoto wao.

“Kuna kipindi nilihuhudhuria mkutano kama huu, nilikuwa sina nguvu za kiume. Nilikuwa nimehangaika sana na nguvu za kiume. Mke wangu hapa naye alikuwa na uvimbe kwenye kizazi kwa miaka tisa.

“Lakini leo hii, nawaambieni tuna watoto watatu ambao wote wanakaribia kumaliza masomo ya sekondari kwenye shule za International. Huyo Mungu aliyeniponya mapungufu ya nguvu za kizazi, atakuponya ndani ya siku tano,” Pasta Ezekiel aliambia kuongamano hilo.
Aidha, Pasta Ezekiel anayefahamika kwa utajiri wake alitoa msaada wa Sh11 milioni kwa ajili ya kusaidia wahanga wa mafurukio katika eneo la Hanang Mkoa wa Manyara, Tanzania ambapo zaidi ya watu 80 walipoteza maisha yao kufuatia mafuriko miezi mitatu iliyopita.

Pasta Ezekiel na mkewe Sarah Wanzu wamejizolea umaarufu kutokana na uinjilisti wao, lakini pia kwa kauli zao tata.

Juzi, Bi Sarah alihoji kuwa hamna maana kubwa mwanamke kujengewa nyumba ya kishua na mume wake kijijini.

Kulingana naye, nyumba inaweza kuwa ni kuta tu na paa lakini la muhimu na msingi kwenye ndoa ni kwa mume na mke kuonyeshana upendo na kumcha Mungu.

Kwake, kujengewa nyumba kijijini si suala la kupewa kipaumbele.

“Hatuna nyumba kule ambako nimeolewa. Tukifika huko, gari ndilo hugeuka kuwa nyumba yetu. Pastor Ezekiel ndiye kifungua mimba na sijalilia nyumba,” aliwaambia waumini juzi.

Mama huyo aliwataka wanawake kuzingatia masuala ya muhimu zaidi kuimarisha ndoa, badala ya kuwaza kujengewa nyumba na waume zao.

“Nyumba sio ndoa na nyumba sio maisha. Mimi sijajengewa. Je, ukijengewa na uachwe, hiyo nyumba nani atakaa humo?” aliuliza.