Chuo Kikuu cha Rongo chafungwa kufuatia vurugu za uchaguzi
NA WYCLIFFE NYABERI
CHUO Kikuu cha Rongo kimefungwa kwa muda usiojulikana na wanafunzi wote kuamuriwa kuondoka mara moja.
Seneti ya chuo hicho iliamua kukifunga kwa sababu ya maandamano ya wanafunzi, ambao walikuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa viongozi wao.
Wanafunzi hao wamekuwa wakizua vurugu tangu Ijumaa wiki jana.
Kufikia Jumanne, walinzi walikiri kukabiliwa na kibarua kigumu kurejesha utulivu.
Wakati wa maandamano hayo, wanafunzi hao waliokuwa na ghadhabu waliharibu mali, huku wakikimbizana na polisi waliofika pale kuwatawanya.
“Seneti katika mkutano uliofanyika Jumanne imeafikia kwamba chuo kikuu kifungwe kwa muda usiojulikana kutokana na fujo zinazoendelea, zinazotokana na uchaguzi wa wanafunzi,” ikasema sehemu ya barua iliyotiwa saini na Naibu Chansela anayeshughulikia Masomo na Masuala ya Wanafunzi, Prof Michael Ntabo Mabururu.
Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Rongo, Prof Samuel Gudu naye alithibitisha kufungwa kwa taasisi hiyo ya elimu ya juu.
“Ndiyo, Chuo Kikuu kimefungwa. Tutatangaza tarehe za kurejelea masomo baadaye,” Prof Gudu ameambia Taifa Leo kwa njia ya simu.
Katika uchaguzi huo wenye utata, viongozi wafuatao walitangazwa washindi:
- Rais – Bw Victor Apicha
- Naibu Rais – Bi Mercy Wangari
- Katibu Mkuu – Ochako Samuel
- Mwakilishi wa Michezo – Reuben Makena
- Mwakilishi wa Maswala ya Akina Dada – Gentrix Iminza