Michezo

Okumbi amwaga sifa kwa timu za Talanta Hela

March 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA TOTO AREGE akiwa BARCELONA, UHISPANIA

TIMU za Talanta Hela za wavulana na wasichana wa chini ya umri wa miaka 19, zitaipeleka Kenya mbele katika ulingo wa soka ikiwa tu vijana hao watapata muda wa kucheza pamoja na pia kujinoa kwa mechi za kirafiki, amesema kocha wa zamani wa Harambee Stars, Stanley Okumbi. 

Okumbi yuko Uhispania na timu za wavulana na wasichana kwa ajili ya Mashindano ya Kombe la Costa Daurada. Timu ya wasichana iko chini ya kocha Jacline Juma.

Baada ya timu ya wavulana kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Akademia ya Nastic katika uwanja wa Nastic mjini Taragona Jumanne, Okumbi alisisitiza umuhimu wa kuwahusisha wachezaji katika mechi za kirafiki na timu ambazo zimekuwa kisoka.

“Ikiwa tunaweza kujaribu kuwa pamoja kwa sababu wengi wao hawako shuleni, basi tutafanikiwa sana linapokuja suala la kukuza soka. Tunahitaji kuandaa mechi za kirafiki zenye ushindani, na mashindano makubwa kila mwezi kwa wiki mbili hadi tatu za mafunzo. Lakini ikiwa tutawaacha baada ya mashindano haya, basi hatutakuwa tumefanya kazi bure. Nimependekeza wazo hili kwa watu husika, natumai watalitekeleza, na hili litatusaidia kukuza mchezo,” alisema Okumbi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Rainbow FC ya Ligi Kuu ya Taifa (NSL).

“Tumecheza mechi nne tangu kuwasili nchini Uhispania mnamo Jumapili, wavulana wanajitahidi sana. Wachezaji wengi hawajakuwa wakifanya mazoezi kwa sababu wako shuleni. Nimekuwa nikijaribu kuwatia moyo kuendelea kujituma kwa kucheza soka,” aliongeza Okumbi.

Ndoto yangu daima imekuwa kucheza Uhispania na nashukuru kwa Mungu kwamba ndoto hii sasa imekuwa ukweli. Hali ya hewa hapa ni tofauti kabisa na nyumbani, lakini tunajitahidi kuikabiliana nayo. Tumepata maarifa mengi kutoka kwa kocha wetu, ambaye amekuwa akituongoza kwa muda wote. Timu hapa nchini Uhispania zinacheza soka tofauti, lakini tumeonyesha kuwa tuko ngangari baada ya kucheza nao. Tutaandikisha historia kupitia Talanta Hela,” alisema kiungo Telena Ochieng.

“Safari imekuwa nzuri, na tunatumai kushinda kombe na kulileta nyumbani. Tutawafunza na wengine yale tuliyojifunza tukiwa Uhispania. Ushindani hapa ni mkali zaidi ikilinganishwa na jinsi tunavyocheza nyumbani,” alisema Valencia Ochieng, mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Wasichana ya Butere, Kaunti ya Kakamega.

Matokeo 

Wavulana 

  • Kenya 3-0 Ce Constanti 0
  • Kenya 4-0 XBuyer
  • Kenya 3-0 Usurbil Football

Wasichana

  • Kenya 3-2 Sporting of Portugal
  • Kenya 4-0 CD Olimpico de Madrid
  • Kenya 4-0 Ce. Jupiter