Serikali yaamuru NCPB ikome kuuza mbolea aina ya NPK inayoshukiwa kuwa ghushi
NA CHARLES WASONGA
KATIBU wa Wizara ya Kilimo Paul Ronoh ameamuru kusitishwa kwa uuzaji wa mbolea kwa jina NPK 10: 26:10 inayotengenezwa na kampuni ya Ken Chemicals ya Thika.
Kwenye barua ya usimamizi wa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) mnamo Jumatano, Dkt Rono alisema kuwa uchunguzi wa nyanjani uliofanywa na maafisa wa serikali umebaini kuwa mbolea hiyo haijatimiza viwango hitajika vya ubora.
“Asasi yako inaombwa kusitisha uuzaji wa wa mbolea hii kwa wakulima kote nchini mara moja,” Dkt Rono akasema katika barua kwa Mkurugenzi Mkuu wa NCPB Joseph Kimote.
Taifa Leo ilipata nakala ya barua hiyo.
“Vilevile, unahitajika kufanya uchunguzi kubaini maelezo halisi kuhusu viungo na madini kwenye mbolea hii kabla ya kurejeshwa katika mpango wa serikali kwa utoaji mbolea kwa bei nafuu,” Katibu huyo akaongeza.
Dkt Rono alisema endapo itabainika kuwa mbolea hiyo haijatimiza matakwa na sifa zilizowekwa, kampuni iliyoitengeneza itaadhibiwa na kulazimishwa kugharimia hasara yote kwa serikali na wakulima.
Hatua hiyo ya kusitishwa kwa uuzaji wa mbolea ya NPK 10: 26: 10 inafuatia ripoti kuhusu malalamishi kutoka kwa wakulima kwamba wanauziwa mbolea feki kutoka kwa mabohari ya NCPB.
Baadhi ya wanasiasa pia wameitaka serikali kuwalipa fidia wakulima ambao wamehadaiwa na kununua mbolea feki na hivyo kupata hasara.
Hata hivyo, mnamo Jumanne, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi alikana madai kuhusu uwepo wa mbolea feki inayouzwa chini ya mpango wa serikali wa kutoa bidhaa hiyo kwa bei nafuu.
“Hakuna mbolea feki inayouzwa sokoni chini ya mpango wa serikali wa usambazaji wa mbolea kwa bei nafuu. Serikali inauza mbolea yenye ubora hitajika kwa wakulima kote nchini,” Bw Linturi akasema.
Alisema hayo alipozuru bohari la NCPB, Elburgon.
Bw Linturi aliwaonya wakulima dhidi ya kujigeuza kama wataalamu wa kubaini ubora wa mbolea.
“Wakulima wetu wakome kutazama mbolea kisha kuhoji thamani yake. Wale wanaoshuku ubora wa mbolea wanapaswa kuwasilisha sampuli zake katika maabara ya serikali ili ifanyiwe uchunguzi,” akashauri.