Habari za Kitaifa

Buriani Rita Tinina

March 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JOHN NJOROGE

MWANAHABARI mashuhuri na aliyekuwa Mhariri katika runinga ya NTV Rita Tinina alizikwa Jumatano nyumbani kwao katika kijiji cha Olokirikirai, Kaunti ya Narok, katika hafla iliyohudhuriwa na wanahabari na watu wa tabaka mbalimbali.

Hafla hiyo haikutumiwa tu kumuomboleza bali kusherehekea maisha aliyoishi yaliyosheheni uadilifu, unyenyekevu na kujitolea katika kazi yake kama mwanahabari tajika.

Wanahabari wenzake, marafiki na jamaa walitumia fursa hiyo kumuenzi kama shujaa wa kupigiwa mfano.

Safari ya mwisho ya Tinina ilianza jana saa moja asubuhi mwili wake ulipochukuliwa kutoka hifadhi ya maiti ya Umash, Nakuru na kusafirishwa kwa mazishi katika kaunti jirani ya Narok.

Msafara wa zaidi ya magari 50 ulisindikiza jeneza lake chini ya ulinzi mkali katika barabara ya Nakuru-Njoro.

Marafiki walimpa heshima na taadhima kwa kuhiari kutumia gari la kifahari la Range Rover jeusi kusafirishia jeneza lake.

Aidha, baadhi yao waliabiri gari hilo ambalo lilipambwa kwa maua maridadi yenye rangi nyekundu, nyeupe na kijivu.

Kuanzia kwa wanahabari wenzake, wanasiasa, waliokuwa wakubwa wake kazini, kila mnenaji alimsifu Tinina kama mwanahabari shupavu aliyependa kazi yake na kutangamana na watu vizuri.

Aidha, alitambuliwa kuwa mtetezi sugu wa haki za wasichana wadogo kutoka jamii ya Maasai kupitia habari kadhaa na makala aliyopeperusha na kuacha taathira kubwa kote nchini.

“Alipenda kusakata densi na muziki, haswa aina ya reggae. Kama kiranja wetu, alikuwa kiongozi mzuri aliyefanya maamuzi yake kwa haki,” ikasema sehemu ya rambirambi iliyosomwa na mwanafunzi mmoja wa zamani wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Maasai ambako Tinina alisomea.

Kwa familia yake, alikuwa binti, dada, mama na hodari katika kutatua changamoto mbalimbali.

Wenzake kazini pia walielezea kujitolea kwake katika taaluma yake.

Walitoa kumbukumbu ya safari yake katika kuboresha weledi wake kama mwanahabari.

Katika risala yake ya rambirambi iliyosomwa na Katibu wa Kitengo cha Habari katika Ikulu Emanuel Talam, Rais William Ruto alimtaja mwendazake kama kielelezo cha uwezo wa taaluma ya uanahabari katika kuleta mabadiliko bora katika jamii.

Dkt Ruto pia alimtaja Tinina kama mwanahabari aliyependa kazi yake na kuifanya kwa moyo wa kujitolea.

“Ni nadra kupata mtu mweledi wa kiwango cha Rita katika taaluma yoyote. Kwake, uanahabari haukuwa kazi tu bali wajibu wake kwa jamii na taifa kwa ujumla. Alipeperusha habari na makala kwa undani na kuhusu masuala yenye umuhimu kwa jamii. Alikuwa mweledi katika kutamba stori,” Rais Ruto akasema.

Tinina alifariki usingizini mnamo Machi 17, 2024.

Kulingana matokeo ya upasuaji, mwanahabari huyo alikuwa akiuagua ugonjwa wa kichomi kikali (Pneumonia).

Tinina ameacha binti kwa jina Mia Malaikah na mpenziwe Robert Nagila.

Miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa Shirika la Habari la Nation (NMG) Joe Ageyo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari katika Shirika la Habari la Royal Media Services Linus Kaikai na Mhariri Msimamizi wa NMG Pamela Sittoni.

Pia walikuwepo wanasiasa kama vile maseneta; Ledama Ole Kina (Narok), Enoch Wambua (Kitui), Edwin Sifuna (Nairobi), Crystal Asige (seneta maalum), madiwani wa Narok na wabunge Babu Owino (Embakasi Mashiriki), Agnes Pareiyo (Narok Kaskazini) na Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini).