Murang’a yapiga marufuku disko matanga, vileo wakati wa uchimbaji kaburi
NA MWANGI MUIRURI
MAHASLA ambao wamekuwa wakipata afueni ya lishe, uji na disko katika matanga ya wafu katika vijiji vya Kaunti ya Murang’a sasa wako taabani baada ya kamati za usalama kupiga marufuku hafla hizo.
Hii ni baada ya kukadiriwa kuwa wengi ambao hufika katika disko matanga usiku na kuchimba kaburi huwa na nia nyingine nje ya kusaidia familia kuomboleza.
Visa vya wizi, ngono kiholela na matumizi ya mihadarati vimetajwa ndio kivutio cha wahuni wanaofika na kukesha palipo na matanga.
“Sisi tumekataa mambo ya disko matanga. Vijana kutoka maeneo jirani hufurika kwa boma la msiba na hawatoi pesa ama kutulia sehemu moja ili kuomboleza na walio kwa majonzi. Huwa wanarandaranda kila pembe ya boma, wengi wakiwa ni majasusi wa mitandao ya wizi,” akasema Mzee James Njoroge wa kijiji cha Muruka kilichoko eneobunge la Kandara.
Alisema kwamba wanajamii katika vijiji vingi katika eneo hilo wamekuja kuelewa kwamba disko matanga huishia kuwa na magenge ya kutambua sehemu ya kutekeleza wizi wa mifugo, mimea au kuvamia ghala ama boma.
“Aidha, tumegundua kwamba baadhi ya vijana ambao hutokea kuchimba kaburi huwa na nia tu ya kula chakula cha bure, hali ambayo huzidisha gharama za kuomboleza,” akasema.
Bw Maina Murigi ambaye ni mwanakamati wa Nyumba Kumi katika eneo la Kihumbu katika eneobunge la Kigumo, alidai kwamba “mahasla hao hutoa bajeti ya chakula ambayo hukaa kama bili ya hospitali”.
Alisema vijana wengi hudai wapikiwe ugali matumbo, chai pamoja na uji huku watundu wengine wakiongeza gharama ya sigara, tumbaku na bangi.
Naye Bi Beatrice Njuguna, ambaye ni mshirikishi wa wanawake katika masuala ya usalama katika kijiji cha Ithanga katika eneobunge la Gatanga, alisema wamechoshwa kuona vijana hao wakizurura ovyo.
“Vijana hao hujitokeza kuchimba kaburi la marehemu wakiwa zaidi ya 100 lakini wanaofanya kazi hiyo huwa ni chini ya 10. Hao wengine huonekana wakirandaranda wakisaka lishe na mihadarati,” akasema Bi Njuguna.
Badala ya kugharimia mlo kwa mahasla hao kwa kisingizio cha kuwatuza kwa kusaidia katika shughuli nzima ya kuomboleza, kamati nyingi za mashinani huonelea ni afueni kulipa vijana kadha kuchimba kaburi.
“Bajeti ya waliofiwa kuchimbiwa kaburi bila malipo huwa kati ya Sh40,000 na Sh70,000 hii ikiwa ni gharama ya upishi wa chakula na uji, sigara na mihadarati. Hata waliookoka hushinikizwa kuwanunulia vijana bangi na tumbaku eti ni kanuni za kutunza waombolezaji vijana,” akasema Bw Moses Ngwiri kutoka Muruka.
Bw Ngwiri aliongeza kwamba kwa sasa bajeti ya kulipa vijana sita kuchimba kaburi la kina cha futi sita na upana wa futi nne ni Sh6,000, hii ikiwa ni afueni kubwa sana kwa bajeti ya mazishi.
“Vijana hao hata tukiwapikia matumbo na ugali na pia tuwape kila mtu kikombe cha uji hatutakuwa tumeenda hasara ya kulisha kongamano la mahasla ambao hujitokeza siku ya uchimbaji kaburi,” akasema Bw Ngwiri.
Uchunguzi wa Taifa Leo umegundua kwamba huu ni mwamko mpya ambao unavuma katika vijiji vingi ili kuhepa gharama na hatari za kugeuza boma la mwendazake kuwa uwanja wa kila mwombolezaji wa kutuzwa mlo, vinywaji na mihadarati haramu.